Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Denmark nchini Tanzania Mhe. Mette Nørgaard Dissing-Spandet jijini Dodoma leo
Machi 18, 2026.
Katika
mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Jafo amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina ya
nchi hizo mbili na inatarajia kuendelea kushirikiana zaidi katika hifadhi ya
mazingira.
Amesema
kuwa Tanzania inashirikiana na Denmark katika kusukuma mbele ajenda ya matumizi
ya nishati safi ya kupikia ambayo itasaidia katika kupunguza kasi ya ukataji wa
miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Kupitia
ajenda hiyo amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kuwa ameonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha asilimia kubwa ya
wanawake wa Tanzania na Afrika kwa ujumla wanatumia nishati safi ya kupikia.
Dkt.
Jafo amesema kuwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tanianchi
(COP28) uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu, Rais Dkt. Samia alizindua Mradi wa Nishati Safi ya
kupikia itakayowasaidia wanawake barani Afrika.
Kutokana
na umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, Waziri Dkt. Jafo amesisitiza
ni wakati sasa Tanzania inahitaji kuwabadilisha wananchi kuachana na matumizi
ya kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.
Ameongeza
kwa kuwashukuru wawekezaji wa nishati safi ya kupikia hususan gesi kwa kuunga
mkono Serikali kwa kutoa mitungi ya gesi kwa taasisi mbalimbali zinazolisha
watu zaidi ya mia moja.
Halikadhalika,
Dkt. Jafo amesema Tanzania inatekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na
athari za uharibifu wa mazingira ambapo ilizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya
mwaka 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(2022-2032).
Kwa
upande wake Mhe. Balozi Dissing-Spandet amemuhakikishia Waziri Jafo kuwa nchi
yake itaendeleza ushirikiano wake kwa Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo
ya mazingira.
0 comments:
Post a Comment