Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuitumia Misikiti kwa shughuli mbali mbali ikiwemo kuanzisha masomo na Darasa ili kupata  jamii iliyo bora.
 
Mhe.Hemed ameyasema hayo wakati akiwasalimia waumini wa Masjid Tawheed Fuoni uwandani alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
 
Amesema ni wajibu wa waumini kuitimia Misikiti kwa kuelimishana masuala mbali mbali hasa kukumbushana kuhusu maadili mema na kusimamia kitabu kitukufu Qur-an ili kupata fadhila za mwewnyezi mungu hapa duniuani na kesho akhera.
 
Aidha, Mhe.Hemed ameeleza kufurahishwa kwake kuona baadhi ya jamii hutumia Misikiti kukusanya takwimu za wana kijiji hasa wenye mahitaji maalum ili kujua namna bora ya kuwasaidia kuondokana na changamoto ambazo zinazowakabili.
 
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewakumbusha wazazi na walezi kusimamia malezi ya watoto wao ikiwemo kuwapatia elimu ya Dini na elimu ya kidunia na kueleza kuwa mtoto mwenye elimu na maadili mema hujenga jamii iliyosalimika na vitendo viovu.
 
Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu ikiwemo kuanzisha kampeni ya kuwarejesha Skuli watoto walioacha kusoma ili kuwapatia haki yao ya msingi ya elimu.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewakumbusha waumini hao kudumisha Amani na Utulivu iliopo nchini ili kutoa fursa kwa Serikali kuweza kuwaletea maendeleo endelevu  wananchi wake.
 
Akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa Sheikh Suweid Ali Suweid amewakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu kuwatendea wema wazazi wawili walio hai na kuwaombea Dua waliofariki kama Uislamu ulivyoeleza.
 
Amesema kuwatendea wema wazazi kunajenga mapenzi baina ya wazazi na watoto pamoja na kujenga jamii bora yenye maadili mema.
 
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top