Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamuwa kujenga Miundombinu ya Barabara ili kurahisisha huduma ya usafiri pamoja na kuongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi nchini.
 
Akiendelea na ziara ya kukagua uhai wa Chama Mkoa wa Kusini Unguja katika Majimbo ya Uzini, Chwaka na Tunguu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kujenga Barabara zote za mijini na vijijini kwa Njia ya Lami ni kuwarahisisha wananchi huduma ya usafiri pamoja na kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.
 
Mhe. Hemed amesema wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wanajishughulisha na kazi za Kilimo na Uvuvi hivyo uwepo wa Barabara hizo kutasaidia mazao ya biashara kufika sokoni kwa wakati yakiwa na kiwango hatua ambayo itarahisisha kuongezeka Uchumi Binafsi na Taifa.
 
Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Mkoa huo ni sehemu moja wapo yenye shughuli nyingi za kitalii hivyo uwepo wa huduma mbali mbali kutapelekea kwa kiasi kikubwa kuongeza Idadi ya watalii sekta ambayo inasaidia kwa asilimia kubwa kukuza uchumi wa Zanzibar.
 
Sambamba na hayo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuunga Mkono juhudi za Serikali kwa kutangaza maendeleo yanayofanywa na Viongozi kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
 
Amesema Serikali zote mbili zinaendelea kuwaletea maendeleo wananchi wake kwa kuzingatia sekta mbali mbali na kueleza kuwa wananchi wana kila sababu ya kuwaunga Mkono Marais wote wawili Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kuwachagua tena kwa kura nyingi ifikapo mwaka 2025.
 
Aidha Mhe. Hemed amewapongeza wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa Majimbo hayo kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kumsaidia Rais Dkt. Mwinyi majimboni kwa kutatua Changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo hayo.
 
Nao viongozi wa Majimbo hayo wameeleza faraja yao kwa maamuzi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuelekeza fedha za Mkopo wa kupunguza athari za Uviko 19 kujengea miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Madarasa ambayo yamepunguza uhaba wa eneo la kusomea na kupelekea wanafunzi kuingia kwa mkupuo mmoja kwa siku.
 
Kwa upande wao wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Mvita Mustafa Ali na Makame Ramadhan Mbanja wamewataka wana CCM kuendelea kuimarisha Chama hicho kwa kusimamia maelekezo yaliyotolewa na Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa maslahi ya chama hicho.
 
Katika ziara hiyo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amepokea zaidi ya wanachama wapya Elfu Moja na Mia tatu (1300) kati ya hao wanachama watano (05) kutoka vyama vya upinzani.
 
Akizungumza kwa niaba yao aliekuwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kati Ndugu. Ali Mbarouk Mshimba ameeleza kuwa ameamua kurudi CCM kutokana na kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 inavyotekelezwa na Viongozi wa Chama hicho.
 
Mapema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ameshiriki ujenzi wa Tawi la CCM Mgeni Haji na kukagua ujenzi wa Tawi la CCM Kikungwi pamoja na Ukumbi wa Mikutano Chwaka.


Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


0 comments:

 
Top