Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amewataka Viongozi na wanachama wa CCM kuwa Wazalendo na kujitolea katika kukijenga na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi. 
 
Akizungumza na Viongozi, wana CCM na wanachama wa Jimbo la Mkoani na Mtambile Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema umefika wakati Viongozi wa ngazi mbali mbali kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana  kukiimarisha na kuinadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. 
 
Amesema umoja na mshikamano ndio nguzo pekee ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kufikia maendeleo ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuyafikia kwa kuwatumikia wazanzibari.
 
Amesema Viongozi wa Vyama vya upinzani wameshaishiwa kisiasa hawana sera zinazonadika wala kutekelezeka badala yake wanatumia majukwaa kwa kuwachafua Viongozi wa CCM na miradi wanayoitekeleza na kuwataka Wananchi kutowasikiliza Viongozi hao badala yake kuendelea kumuunga mkono  Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi anazoendelea kuzichukua nchini .
 
Amesema kuwa Serikali itafikisha umeme katika kijiji cha Kikunkwe ambacho ni kijiji pekee katika Wilaya ya Mkoani ambacho hakijafikiwa na huduma hiyo sambamba na kuwaahidi wananchi wa Mkoa huo kuwa Serikali itajenga Dakhalia katika Skuli ya Sekondari ya Uweleni jambo ambalo litatatua changamoto ya wanafunzi kwenda na kurudi majumbani na kusaidia kusongeza ufaulu kwa wanafunzi na kupunguza vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali karibuni itaanza ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo Mkoa wa Kusini Pemba ambapo kipaumbele cha ajira ni kuwaajiri vijana wa Mkoa huo hatua ambayo itasaidia kukuza kipato na kuweza kujikimu kimaisha
 
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Matar Zahor Masoud ameeleza kuwa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwafikishia huduma wananchi wake pasi na upendeleo ili kumaliza tatizo la changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo.
 
Amesema kuwa tayari Serikali imeshachimba visima kumi na saba (17) Mkoa wa Kusini Pemba kati ya hivyo visima kumi na moja (11) vimechimbwa Wilaya ya Mkoani pamoja na kukamilika zoezi la usambazaji wa mabomba ya maji ili kufikisha huduma hiyo kisiwa Panza na makoongwe ili kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama mkoani humo.
 
Kwa upande wake Muwakilishi wa Viti Maalum kupitia Jumuiya ya wazazi Mhe. Azza Januari Joseph ameeleza kuwa Serikali ya mapinduiz ya Zanzibar imefanya jitihada mbali mbali kukuza sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa skuli za ghorofa na madarasa na kuwataka wazazi na walezi kuto mashirikiano na walimu katika kusimamia malezi kwa watoto ili kupata taifa lenye elimu na maaadili mema
 

Awali Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amekagua mradi wa milango mine ya maduka ya Tawi la CCM Mkanyageni na kueleza kuwa mradi huo utasadia kupata kipato kitakachopelekea Tawi hilo kujiendesha kwa shughuli mbali mbali na kuacha utegemezi wa Viongozi wa CCM.

0 comments:

 
Top