Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka wazazi na walezi kulisimamia suala la mmongonyoko wa maadili kwa vijana ili kupata vijana wenye maadili mema na wenye heshima.
 
Akiwasalimu waumini wa Masjid Ibrahim Mombasa kwa Mchina katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, Alhajj Hemed amesema ni jukumu la kila mzazi au mlezi kumpatia kijana wake malezi mema ili kuweza kuirejeshea heshima nchi kwa kupata kizazi chenye maadili mema kama ilivyokuwa zamani.
 
Alhajj Hemed amesema wazazi na walezi wanajukumu kubwa sana la kuwasimamia vijana hususan wale wenye umri chini ya miaka 18.
 
Sambamba na hilo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa jamii kwa sasa imeacha malezi ya zamani na kuiga malezi ya sasa jambo ambalo linasababisha kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mmongonyoko wa maadili ya wazanzibari, hivyo ni vyema wazazi kuhakikisha wanawalea watoto wao kwa malezi yenye maadili mema.
 
Aidha, Alhajj Hemed amewataka  Wazazi kuitumia Misikiti kujadili mambo mbali mbali yaliyomo katika jamii zao ikiwemo kukumbushana malezi pamoja na kuyarejesha maadili ya kizanzibari.
 
Kadhalika, amewataka wazazi na walezi kuwazoesha vijana kufanya Ibada na matendo mema pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu ili kupata maisha mazuri Duniani na  Akhera.
 
Akitoa Khutba ya Sala ya Ijumaa Sheikh Abdallah Ali Abeid amewataka Waislamu kuishi maisha kama aliyokuwa akiishi Mtume Muhamad (S.A.W) katika kumcha M/Mungu kwa kufata misingi ya Qur-an na Sunna, kwani kufanya hivyo kutawasaidia kuishi maisha mazuri hapa duniani na kesho akhera.
 
Aidha ameeleza kuwa ni wajibu wa waumini wa Dini ya Kiislamu kuwa waaminifu na kuacha kufanya hiyana pale ambapo wataaminiwa na wenzao ili kuishi maisha yaliyo bora hapa duniani.
 
Imetolewa na kitengo cha habari (OMPR)

0 comments:

 
Top