Juhudi za wahariri kutoka vyombo mbali mbali vya habari nchini zimesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuleta mabadiliko katika matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo katika Mkutano wa wahariri wakuu wa vyombo vya habari katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani uliofanyika ukumbi wa shekh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Amesema wahariri wakuu wana jukumu la kupitisha na kuweka sawa maandishi yote ndani ya Vitabu, Magazeti na majarida hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza lugha ya kiswahili .
Aidha Mhe. Makamu mewataka wahariri kulinda Maadili ya kazi zao katika kuyaibua mambo mbali mbali yasiyo endana na mika, tamaduni na silka zetu bila ya kumuonea Mtu au Taasisi fulani.
Sambamba na hayon Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa kuna fursa nyingi zinazopatikana katika lugha ya Kiswahili na kuwataka wenye ujuzi wa Lugha hiyo kuchangamkia fursa hizo ikiwemo ukalimani, tafsiri, uhariri, uandishi na utangazaji wa habari pamoja na ufundishaji wa Lugha hiyo kwa wageni.
Ameelezea na kufurahishwa kwake kwa kuona kupitia Baraza la Kiswahili Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kuweka mikakati katika Nchi mbali mbali ya kukizungumza na kukieneza kiswahili ikiwemo Ujerumani, Uholanzi, Italia, Nigeria, Nchi za falme za kiarabu, Malawi, Rwanda na Zimbabwe hatua ambayo ni dhahiri ya umahiri wao katika kutangaza Lugha hiyo.
Ameeleza kuwa mbali na juhudi hizo tayari Nchi zisizopungua Thalathini na Nane (38) kupitia Redio na vituo vya Televisheni vinarusha matangazo yake kwa Lugha ya Kiswahili.
Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amelitaka jukwaa la wahariri kushirikiana na Mabaraza ya Kiswahili nchini kuhakikisha vyombo vya habari vinatumia kutumia kiswahili fasaha na Sanifu .
Kwa kuzingatia upeke wa lugha ya kiswahili Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeamua kuifanyia marekebisho Sheria ya Habari ili iendane na Mabadiliko yanayotokezea katika Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe Tabia Maulid Mwita ameeleza kuwa Serikali ina Mkakati wa kukifanya Kiswahili kuwa ni bidhaa itakayowanufaisha wataalamu na Taifa kwa ujumla ikiwemo kupeleka walimu kusomesha Kiswahili nje ya Tanzania pamoja na kuwakaribisha wageni kusoma Lugha ya Kiswahili ndani ya Tanzania.
Aidha Mhe. Tabia amewataka wahariri wakuu kukemea tabia ya wachache wanaotumia Misamiati kinyume na maana zilizokusudiwa ili kudhibiti ufasaha wa Lugha ya Kiswahili.
Nae Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Khamis Mwinjuma ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuchukua jitihada mbali mbali katika kuhakikisha Lugha ya Kiswahili inakuwa ni Nembo ya Taifa la Tanzania.
Amesema ni wajibu wa wananchi kuhakikisha wanaitangaza Lugha ya Kiswahili ikiwemo kuibua Utalii wa Lugha ya Kiswahili ili kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanatumua fursa zitokanazo na Lugha hiyo.
Akitoa maelezo kuhusu Jukwaa hilo Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa Bi Consolata Mushi ameeleza kuwa Jukwaa hilo litakuwa ni chachu ya kupunguza changamo to za Kiswahili zinazojitokeza katika Vyombo mbali mbali vya Habari.
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment