SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itawahamasisha walimu wa skuli za Serikali kwa kuwazawadia kwa mujibu watakavyotoa ufaulu wa daraja la juu zaidi kwa wanafunzi wanaowasimamia kwenye masomo yao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo, ukumbi wa Tibirinzi, Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba, kwenye hafla fupi ya kuwazawadia kompyuta aina ya “laptop” wanafunzi wa kidato cha nne na sita waliofanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Ikulu, Zanzibar anapojumuika nao kwenye chakula cha pamoja kila baada ya wanafunzi hao wanapomaliza mitihani yao ya taifa na kupata ufaulu mzuri.

Alisema Walimu wanahitaji motisha maalumu ili kuwashajihisha kuboresha mfumo wa Elimu Zanzibar kwa kuleata mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo ikiwemo kuongeza ufaulu mzuri.

Dk. Mwinyi alieleza Serikali imejikita kwenye kuimarisha miundombinu kwa skuli zote ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi wengi ikiwemo kuondosha mikondo kwa skuli zote za Unguja na Pemba kwa kuendelea kujenga skuli za ghorofa za msingi na Sekondari ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kuhudhuria masomo ya madrasa wakati wa jioni kwa kuwa na mkondo mmoja.

Akizungumzumzia ufaulu wa wanafunzi wengi, Rais Dk. Mwinyi alisema mara zote amekua akiwaahidi zawadi nzuri zaidi kwa wanafunzi hao kama hamasa ya kuwashajihisha wengine kufanya vizuri hali aliyoieleza kuleta tija katika kuongeza ufaulu nchini.

Alisema adhma ya Serikali ni kuondoa ufauli wa daraja sifuri na daraja la nne kwa kuweka mkazo kwenye kuongeza kuongeza ufaulu Zaidi.

Naye, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulgulam Hussein kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Lela Muhamed Mussa alisema wizara imeongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa Sekondari kutoka asilimia 4.6 mwaka 2021 hadi kufikia 26% kwa mwaka 2023 hali aliyoitaja mafanikio makubwa kwa sekta ya Elimu na kueleza kuwa hamasa zimesaidia sana kuongeza ufaulu huo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu Mfanyabiasha maarufu Zanzibar, Said Bopar aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi za kuimarisha huduma za jamii nchini zikiwemo sekta za Afya na Elimu na kueleza kuwa hamasa wanayotoa kwa wanafunzi hao ni ya kuungwa mkono na kila mmoja.

Bopar alieleza hayo alipokabidhi laptop 150 kwenye viwanja vya kufurahishia watoto, Tibirinzi Pemba, kwa wanafunzi walifanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa kwa kidato cha nne na sita ikiwa ni ahadi aliyoitoa kwa wanafunzi hao na juhudi zake za kuiungamkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, aidha aliahidi tena kompyuta nyengine 150 kwa wanafunzi watakaofanya vizuri Zaidi kwenye masomo yao.

Miongoni mwanafunzi waliowakilisha wenzao kupokea kompyuta hizo ni Hajra khamis Ali, Haitham Omar Abdallah, na Salum Ahmeid Nassor wote kutoka skuli ya Sekondari ya Fidel Casro na Lukman Mohamed Ali kutoka skuli ya Sekondari Chasasa, Wete Pemba

 IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR

0 comments:

 
Top