Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika katika viwanja vya hoteli Verde Mtoni Jijini Zanzibar.
Amesema Serikali iliyopo madarakani hivi sasa inaendeleza jitihada kwa wazee miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuendelea kuwatunza wazee wasiokuwa na jamaa wala rasilimali katika makao maalum Sebleni na Welezo kwa Unguja na Limbani kwa upande wa Pemba.
Dkt. Mwinyi amesema, kwa sasa kuna jumla ya wazee Sitini na Sita (66) kwa Unguja na Pemba na Serikali inatoa huduma zote muhimu kwa wazee hawa ikiwemo Chakula, Malazi, Mavazi, Matibabu pamoja na kuwapatia posho.
Aidha, Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wanajamii kwa kuwataka kutokwepa majukumu ya kuwalea wazee wao na kuwataka kuacha tabia ya kuwapeleka kulelewa katika makao ya wazee kwani wazee wanahitaji mapenzi na huruma kutoka kwa watoto wao na jamii inayowazunguka. “ni vyema wanajamii kuwalea wazee katika familia zao kama ambavyo wazee hao walivyotumia muda, nguvu na rasilimali zao kuwatunza wakati wakiwa madogo” amesema
Sambamba na hayo, Rais Mwinyi amesema Serikali imeanzisha mpango maalum kwa kuwapatia kuanzisha pencheni jamii wazee wote ambao wametimiza umri wa miaka sabiini (70) tokea mwaka 2016 ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa sera na hifadhi ya jamii ya mwaka 2014 ambayo moja wa changamoto ni usalama wa kipato.
Amesema, hadi kufikia mwezi wa Septemba mwaka huu jumla ya wazee Elfu Ishirini na Nane, Mia Saba na Sita (28,706) kwa Unguja na Pemba wamepatiwa Pensheni Jamii. “pensheni hii inawasaidia wazee kuimarisha maisha yao na wapo wazee wengi wamefaidika na pensheni hii na wapo wazee wengine wanawahudumia familia zao hadi hii leo” amesema
Hata hivyo, Dkt. Mwinyi amesema kuwa takwimu za utafiti wa mapato na matumizi ya kaya 2014/2015 zinabainisha kwamba asilimia kumi na moja nukta mbili (11.2%) takwimu hizi zinaonesha kuwa bado jamii inawapa mzigo wazee kwa kuendelea kuhudumia familia zao.
Dkt. Mwinyi amewataka wafanyakazi wa pensheni jamii, wazee na wanajamii kutumia vizuri mpango huu kwa kuwasaidia wazee wenye sifa kusajiliwa na pia kuwasaidia kupata fedha zao kwa kila mwezi, katika kuimarisha na kuhakikisha kuwa mpango huu unakuwa endelevu serikali imeandaa sheria ya wazee ambayo imekuwa na mfumo wa kisheria ili uweze kuwasaidia katika maisha yao.
Amesema Serikali imeanzisha mfumo wa kuhifadhi taarifa za wazee ambao utarahisisha usajili wa wazee, utunzaji wa kumbukumbu pamoja na mfumo wa malipo kwa ujumla hivyo, mfumo huu umeunganishwa na mkonga wa Taifa ili kuweza kumtambua mzee aliyefikia umri wa kuingia kwenye malipo ambapo mfumo huu ni wa mwanzo kwa Nchi za Afrika kwani unatumia alama za vidole ambapo serikali inashirikiana na mashirika ya UNICEF na HELPAGE ili kusimamia na kuimarisha mfumo huu.
Mhe. Rais wa Zanzibar amesema kuwa Serikali inafanya kila juhudi kupitia wizara ya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto kwa kushirikiana na Jumuiya za wazee na mabaraza ya wazee katika kusimamia maendeleo ya wazee nchini, amesema kuwa hadi sasa kuna jumla ya mabaraza mia mbili na sitini na nane (268) yameshaundwa na mengine yanatarajiwa kuundwa katika shehia zote mia tatu thelathini na nane (388) na kwa sasa serikali imeanza kutoa vitambulisho maalum vya kuwasaidia wazee kupata huduma muhimu za kijamii kwa urahisi zaidi na vitambulisho (689) tayari vishachapishwa na leo watakabidhiwa wazee na vyengine 2314 vitatolewa hivi karibuni.
“Wazee wanakabiliwa na matatizo mengi ya kiafya ambapo maradhi kama sindikizo la damu, sukari, maradhi ya viungo na macho yamekuwa yakiwaathiri sana na kupunguza uwezo wa kufanya kazi na kujipatia kipato” amesema
Hata hivyo, Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF imefanya marekebisho ya sheria na kuimarisha pensheni za wastaafu kwa wastani wa asilimia 40%, pia kupitia mwaka huu wa fedha wa 2022 mfuko utafanya tena tathmini ya uhimilivu wa miaka 50 (actuarial evaluation) ikiwemo uwezekano wa kuwaongezea kiwango cha pesheni kwa wazee wastaafu.
Amesema kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakiikisha kuwa tunaunga mkono jitihada za Serikali na Wadau wengine kuhakikisha Hali, Ustawi na Hadhi ya Wazee nchini inaimarika siku hadi siku.
Sambamba na hayo aliwakumbusha wazee juu ya wajibu wao wa kuleta ustawi mzuri wa jamii kwani imeshuhudiwa kuwepo kwa mmong’onyoko mkubwa wa maadili unaolikabili Taifa. Hivyo, wazee wana nafasi kubwa ya kusimamia na kudumisha mila, desturi, silka na tamaduni za kizanzibari ambazo zimekuwa zikiipatia sifa nchi yetu.
“Mila desturi na silka zetu zimekuwa zikijenga misingi imara ya upendo mshikamano Heshima, Utii, Nidhamu, Amani na Utulivu katika nchi yetu ni jambo la kusikitisha kuona mambo haya yanatoweka kwa kasi kubwa hivyo wazee wangu hakikisheni mnakuwa mstari wa mbele kutumia maarifa, ujuzi na uzoefu wa miaka mingi mlioishi kusimamia malezi ya viajna wetu ili wawe vijana mwenye malezi mema na kutoa mchango katika ujenzi wa taifa letu na kukemea vitendo vyote vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto” amesema
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. RIZIKI PEMBE JUMA amesema kuwa wizara inafanya kazi kubwa yakuhakikisha wazee wanaishi katika maisha ya heshima kama wanaadamu wengine jambo ambalo limedhihirika katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambazo zimeeleza kwa uwazi haki za binaadamu ikiwa ni pamoja na Wazee.
Hivyo, ameahidi kuwa Wizara kwa kushirikiana na taasisi nyengine za Serikali na mashirika binafsi kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazowakabili wazee nchini.
Aidha, Mhe. Pembe amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Jumuiya za Wazee zimekuwa zikifanyakazi kubwa kuhakikisha Wazee wanaishi katika maisha yaliyobora na yastaha kwa kutoa elimu kwa jamii kwa lengo la kuwalinda na kuwatunza.
Nae Bi SHAFIKA MOHAMMED kwa niaba ya wazee wenzake amesema licha ya jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kuwaenzi wazee bado wazee wa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta mbali mbali ambazo zinawakwaza katika kufikia malengo yao.
Akizitaja baadhi ya changamoto hizo amesema; mafao yanayotolewa kwa wazee kupitia pensheni jamii bado ni kidogo mno kutokana na hali ngumu za maisha; huduma za afya kwa wazee bado hazijazingatiwa vya kutosha ikiwemo upatikanaji wa dawa na madaktari.
Changamoto nyengine amesema; kuwepo kwa lishe duni kwa wazee hasa wanaoishi vijijini, kuzalilishwa kwa tuhuma za uchawi pamoja na kukosekana kwa mfuko maalum wa maendeleo ya wazee utakaosaidia utatuzi wa changamoto zao mbali mbali.
Hivyo, wameishauri Serikali kushusha umri unaowawezesha kupatiwa pensheni kuwa miaka 50 badala ya 70 ambao unazingatiwa kwa sasa, Aidha, kuongeza kiwango kinachotolewa katika mpango wa pensheni jamii, kuanzishwa kwa dirisha maalum la kuwasaidia wazee katika sehemu zinazotolewa huduma kama Hospitali, Benki na maeneo mengine.
Nao wawakilishi kutoka mashirika binafsi wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika suala la kuanzisha mfuko wa pensheni jamii ya wazee jambo ambalo limeiheshimisha Tanzania na kuzifanya nchi nyengine kuja kujifunza jambo hilo.
Wamesema, kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar ili kuona maslahi ya wazee yanaendelea kuimarishwa nchini.
Ali Moh’d
Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment