Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Serikali Mkoa wa Mjini Magharibi kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ujenzi wa madarasa Thalathini na Sita (36) katika Mkoa huo.

Mhe. Hemed ametoa agizo hilo wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua miradi inayoendelea kujengwa kwa fedha za Ahueni ya uviko 19 katika Wilaya ya Magharibi A.

Amesema kuwa Serikali imeelekeza kujengwa madarasa 84 katika Wilaya hiyo na kueleza kuwa ni jukumu la Serikali ya Mkoa huo kuhakikisha wanasimami upatikanaji wa maeneo ya kujenga na kuwakabidhi wakandarasi ambao ni Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) kuanza kazi ndani ya siku kumi.

Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa kukamilika kwa madarasa hayo kutaweza kuwasaidia Walimu kufundisha katika mazingira mazuri na kuongeza ufaulu kwa WSanafunzi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amelipongeza Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar  (JKU) kwa hatua nzuri waliofikia katika ujenzi wa madarasa hayo na kuwasihi kusimamia mkataba ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.

Akigusia changamoto ya Mabati Mhe. Hemed ameruhusu wakandarasi wa Madarasa kutumia mabati waliyokuwa nayo ambayo ni ya kiwango cha hali ya juu ili kudhibiti muda wa ujenzi huo usiweze kuchelewa.

Kuhusu Hospitali ya Wilaya ya Magharibi A inayojengwa eneo la Mbuzini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa kukamilika kwa Hospitali hiyo kutapunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospital ya Rufaa Mnazi Mmoja na kueleza kuwa Hospital hiyo itakuwa na vifaa vya kisasi na vya kutosha na kuhakikisha kuwa huduma zote za msingi zitapatikana.

Nae Mkuu wa Wilaya Magharibi A Mhe. Suzan Peter Kunambi ameeleza kuwa ujenzi wa Hospital ya Wilaya ni kilio cha muda mrefu cha Wananchi hivyo Hospital hiyo inatarajiwa kuhudumia  Wananchi wa Shehia 31 za Wilaya hiyo na Wilaya nyengine.

Aidha amesema kukamilika kwa Hospital hiyo kutatoa chachu ya maendeleo Nchini katika kuboresha huduma za Afya Nchini.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kihinani Msingi Bi Mwanajuma Makame Issa ameeleza kuwa ujenzi wa Madarasa katika Wilaya hiyo kutapunguza masafa kwa Wanafunzi kufata elimu masafa ya mbali na kueleza kuwa hatua hiyo itapelekea kupunguza matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top