Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamvumilia yoyote atakaejihusisha na matendo ya udhalilishaji kwa lengo la kumaliza kabisa tatizo hilo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt Hussein Ali Mwinyi ametoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa Niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akizindua Kongamano la Nane la kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Amesema Serikali imejipanga na inaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wanaojihusisha na matendo hayo ambayo yanaiathiri jamii hasa kwa vizazi vijavyo.

Dkt Mwinyi amesema imefika hatua kwa wananchi kuacha muhali na kutowaonea huruma wafanyaji wa vitendo hivyo ili kuisaidia Serikali katika kusimamia kesi za matukio hayo ya udhalilishaji.

Aidha Rais Dkt Mwinyi ameiasa jamii iendelee kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuwafichua wahusika wa matendo hayo kwa pamoja na kutoa ushahidi unapohitajika ili sheria iweze kufata mkondo wake.

Pamoja na hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewataka waumini hao kuiga kigezo chema na Mtume Muhammad (S.A.W) ambae alikuwa akikemea kwa maneno na vitendo juu ya udhalilishaji wa wanawake na watoto.

"Mtume Muhammad (S.A.W) alikuwa akikerwa na matendo yote ya kuwadhalilisha wanawake na watoto na kufikia kuwakaripia wale wote wenye tabia na mienendo hiyo"  Alisema Dkt Mwinyi

Sambamba na hayo Rais Dkt Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwaasa waumini kujiandaa kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuzidisha Ibada na kuacha yote yaliyokatazwa na Sheria yetu.

" Naomba tukumbushane kwamba Mwezi Mtukufu wa Ramadhan upo mlangoni na ni wajibu wetu kujiandaa kuupokea namna bora kabisa ya kuupokea ugeni huu ni kuzidisha Ucha Mungu kwa kufanya Amali njema na kuacha yale yote tuliyokatazwa" Dkt Mwinyi.

Pia Rais Dkt Mwinyi amewaasa wafanyabiashara kujitahidi kuwaonea huruma waumini katika Mwezi wa Ramadhan kwa kuweka tahfifu bei ya bidhaa na kukemea tabia ya baadhi ya Wafanyabiashara kupandisha bei kiholela ili kuepuka chumo la haramu.

Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kujikita katika Ibada kufikia Daraja la Uchamungu ambali ndio lengo la kuweko kwa funga ya Ramadhani.

Amesema Uislamu umeeleza kuwa ni hasara kubwa kwa Muumini ambae amediriki Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kutosamehewa madhambi yake.

Nae katibu Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Relief and Development Foundation (ZARDEFO) Ali Muhammad Haji ameeleza kuwa lengo la kuandaa Kongamano hilo ni kuwaweka tayari waumini kuweza kuukabili Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuwakumbusha waumini kuweza kujikita katika Ibada katika Mfungo mzima wa Mwezi wa Ramadhan.

Akiwasilisha Mada katika Kongamano hilo  Alhabyb Muhammad Bin Hussein Alhabshy kutoka Seuni Hadhramut Nchini Yemen ameeleza kuwa ili kumaliza tatizo la Udhalilishaji ni vyema waislamu kurudi katika Sheria ya Allah Mtukufu.

Mada kuu katika kongamano hilo ni athari za udhalilishaji katika uislamu.

ABDULRAHIM KHAMIS

OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR

0 comments:

 
Top