Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewaagiza makatibu wakuu kusimamia fedha za miradi ya ahueni ya uviko 19 ili kuhakikisha inakamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Mhe. Hemed ametoa agizo hilo katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Serikali haitoridhia kuona miradi hiyo inavuka muda uliopangwa katika Mikataba kwa kisingizio cha wakandarasi kuchelewa kupata fedha kwa urasimu wa watendaji wa wizara husika.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Fedha zimeshatengwa kwa ukamilifu ili kuweza kukamilisha miradi hiyo kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar.
Aidha makamu wa pili ameeleza kuwa ni vyema kuepuka matumizi yasiyo na ulazima hivyo fedha zitakazo baki katika miradi hio zielekezwe katika miradi mengine kwa manufaa ya Wananchi.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka viongozi hao kuhakikisha Wakandarasi wa miradi hio hawapati changamoto ya aina yoyote ili kuwarahisishia kazi zao kuweza kukamilika kwa muda uliopangwa.
Pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kukipongeza kikosi cha Zima Moto na uokozi Zanzibar kadri wanavyoendelea na ujenzi wa Madarasa katika Mkoa huo na kueleza kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya nane ni kuhakikisha wakandarasi wazawa wanasimamia miradi hiyo kizalendo.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed ameutaka uongozi wa Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuhakikisha wanakaa pamoja ili kuona njia bora ya kusimamia ujenzi wa karakana zinazojengwa na Serikali zenye lengo la kusaidia Wananchi kuweza kupata huduma mbali mbali kwa urahisi zaidi.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 inayoelekeza kutoa huduma bora za Afya, elimu, maji safi na salama, miundombinu, pamoja na maeneo mengine ambapo hadi sasa hatua iliyofikia katika ujenzi wa miradi hiyo ni ya kuridhisha.
Aidha Mhe. Hemed ameziagiza Halmashauri za Wilaya kuhakikisha wanafatilia na kusimamia kwa kina maendeleo ya miradi hiyo na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wakandarasi wanazifikisha sehemu husika.
Kwa upande wa Skuli zinazofanyiwa ukarabati Mhe. Hemed ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha wanatafuta Fedha kwa ajili ya kuezeka Skuli ya Bambi ambayo Paa lake linavuja.
Kwa Upande wake Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi RASHID MZEE ABDALLA amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa ujenzi wa madarasa ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja yatakamilika kwa muda uliopongwa ili kutoa fursa kwa wanafunzi kukaa katika mazingira mazuri ya kusomea.
Aidha Kamishna Rashid amesema majengo hayo yanayojenga na kikosi hicho atahakikisha yanamaliza kwa wakati na kwa kiwango cha hali ya juu ili kuondosha changamoto ya sehemu za kusomea kwa wanafunzi wa Mkoa huo na Mikoa jirani.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Serikali ya Mkoa imefurahishwa kwa hatua iliyofikia Miradi hiyo na kumuhakikishia kuwa Viongozi wa Mkoa huo wataendelea kusimamia Miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Pia Mhe Rashid amesema kuwa atahakikisha Serikali ya Mkoa inasimamia Miradi hio ili imalizike kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa ili kuondoa changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo.
ABDULRAHIM KHAMIS
OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR
0 comments:
Post a Comment