Wananchi wametakiwa kulinda miundombinu inayojengwa na Serikali ili iweze kuleta tija kwa maendeleo ya watanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akizindua Mnara wa Mawasiliano ya 4 G katika kijiji cha Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Serikali imedhamiria kusogeza huduma za Mawasiliano karibu na makaazi ya wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa maendeleo.
Amesema Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimejipanga kuweka fedha maalum zitakazotumika kwa ajii ya kuwasogeza huduma mbali mbali za kijamii wananchi wake.
Aidha mhe. Hemed amesema Azma ya Serikali zote mbili ni kuhakikisha kuwa viongozi wanasimamia vyema fedha za Serikali hatua ambayo inarejesha nidhamu kwa watumishi na kuwajibika katika majukumu yao kwa maslahi ya taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania TTCL kufikisha huduma katika maeneo mbali mbali nchini ni katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kueleza kuwa jambo hilo ni la msingi kwa watanzania wote.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka wananchi kutumia vyema minara hiyo ili kuongeza kasi za kimaendeleo na kuwataka kuzalisha fursa mbali mbali za ajira zinazopatikana kupitia mitandao.
Pamoja na Mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali itaendelea kusogeza huduma za kijamii karibu na maeneo ya wananchi ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za muhimu ikiwemo huduma za simu.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Rahma Kassim Ali ameeleza kuwa Wizara itahakikisha minara hiyo inabaki salama na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa yoyote ataebainika kuharibu miundombinu hiyo.
Aidha Mhe. Rahma ametumia fursa hiyo kukemea tabia ya baadhi ya wasiopenda maendeleo kutumia njia ya simu kutapeli wananchi na kuwataka wananchi kutoa taarifa sehemu husika ili kuwadhibiti wahalifu hao.
Nae waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nauye amesema Wizara kupitia Mfumo wa Mawasiliano itaendelea na usambazaji wa Minara ambapo minara zaidi ya hamsini itajengwa Zanzibar.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania TTCL Ndugu Waziri Ndimba ameeleza kuwa ujenzi wa Mnara huo ni katika mpango wa TTCL kufiksha huduma za Mawasiliano Mjini na vijijini.
Aidha amesema uwepo wa minara ya Mawasiliano inarahisisha kukuwa kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment