Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito kwa viongozi wa taasisi mbali mbali za Serikali na binafsi kushiriki kikamilifu katika kupiga vita rushwa na uhujumu uchumi katika nchi na taasisi zao.

Ametoa wito huo wakati akiendesha Kikao cha kwanza cha 2022 cha Kamati ya Kitaifa ya kuratibu Mkakati Shirikishi wa kuzuwia Rushwa na Uhujumu uchumi Zanzibar  kilichofanyika katika  ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kikwajuni Jijini Zanzibar.

Mhe.Hemed ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kuratibu mkakati shirikishi wa kuzuia rushwa na uhujumu uchumi amesema licha ya Serikali kupambana na rushwa bado inakabiliwa na changamoto hiyo katika maeneo mbali mbali ambapo kunahitajika juhudi kubwa za viongozi na wakuu wa Taasisi ili kumaliza kabisa tatizo hilo nchini.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Kamati hiyo ina nafasi kubwa katika kuisaidia Serikali katika kupambana na janga hilo na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi ili kuwasimamia  vyema  wanaowaongoza.

“Tuhakikishe tunasisitizaa tunaowaongoza na jamii waache vitendo hivi vinarudisha nyuma, na tuanze kujisafisha katika Ofisi zetu” amesema Mhe. Hemed

Sambamba na hayo Mhe Hemed amesema kikao hicho ni sehemu ya kumaliza kabisa tatizo hilo ambapo kikao hicho sehemu pekee ya kuratibu namna bora ya kupambana na janga hilo ili kusaidia kukuza uchumi  wa nchi.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inaendeleza mapambano dhidi ya Rushwa ambapo haitomvumilia mtu yoyote atakaejaribu kushiriki kwa uhujumu wa uchumi kwa namna yoyote.

Akigusia Mkakati huo Mhe. Hemed amesema kuna haja kwa viongozi wote wa Serikali kuweza kuufahamu mkakati huo  ambao umeeleza kwa kina namna bora yakuzuia rushwa nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa azma ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussen Mwinyi ni kumaliza kabisa tatizo la rushwa na uhujumu wa uchumi nchini.

Akigusia uwajibikaji Mhe. Hemed amewataka viongozi hao kuacha muhali katika maeneo yao ya kazi na kueleza kuwa hali hiyo ndio inayorejesha nyuma utendaji wa kazi kwa viongozi hao.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambae ni Waziri na Nchi Afisi ya Rais Katibu Sheria, Utumishi na Utawala bora Mhe. Harun Ali Suleiman amesema kuwa ni vyema kuendeleza kutoa taaluma  kwa jamii ili kuweza kusaidia kumaliza kabisa tatizo la rushwa nchini.

Mhe. Harun ameeleza kuwa Wizara ina mpango wa kupitia mkakati uliowekwa na kushauri namna bora ya kuandaa mkakati mwengine wa miaka ijayo.

Akiwasilisha Mada juu ya Mkakati Shirikishi wa kuzuwia rushwa na uhujumu Uchumi Afisa Elimu kwa Umma kutoka Mamlaka ya kuzuwia Rushwa na uhujumu wa Uchumi Zanzibar Ndugu Ftari Mzee Ali ameeleza kuwa lengo la kuwepo kwa mkakati huu ni kusimamia na kuwataka viongozi hao kila mmoja awajibike katika nafasi yake ili kumaliza tatizo la Rushwa Zanzibar

Hata hivyo afisa huyo amesema kuwa mashirikiano ya Taasisi mbali mbali zikiwemo Mamlaka ya kuzuwia rushwa na uhujumu uchujumu (ZAECA) ,mdhibiti na Mkakuguzi Mkuu wa hisabu za Serikali (CAG) , mkurugenzi wa mashtaka (DPP), Jeshi la Polisi na nyenginezo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha tatizo hilo nchini.


Abdulrahim khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top