Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi wa Tanzania ili kuongeza Imani zaidi kwa wananchi hao.
Mhe. Hemed ameyasema hayo katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa Mfuko huo wa Tanzania bara na zanzibar kilichofanyika Ofisini kwake Vuga.
Amesema kumekuwa na changamoto kadhaa zinazoukabili mfuko huo ambazo zinapelekea kuchelewa kwa Stahiki za wanufaika wa mradi huo hali ambayo inakosesha utulivu wanufaika wa mradi huo.
Amesema ni vyema watendaji wa pande zote mbili za Muungano kuwa na kawaida ya kukutana mara kwa mara ili kujua namna bora ya kuboresha mradi huo ili uweze kufikia malengo yaliokusudiwa .
Mhe. Hemed amesema Mradi huo unawagusa wananchi walio wengi wenye hali duni ambao huweza kujikwamua kimaisha na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii katika vijiji vyao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka watendaji hao kurekebisha mfumo wa wanufaika ili uweze kurahisisha kuwatambua na kuwafikia wananchi kwa urahisi na kuwaagiza kuweka watendaji watakaowajibika katika kusimamia mfumo huo.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewapongeza watendaji hao kwa kuonesha moyo wa kizalendo na kuongeza kuwa Zanzibar ni sehemu ya kupigiwa mfano kwa kufanya vizuri na kueleza kuwa SMZ inataraji kuona inafanya vizuri zaidi kwa kipindi kijacho.
Mhe. Hemed amesema wananchi wana Imani na matumaini makubwa na mradi huu ambao Serikali imeanzisha ili kuwasaidia kujikimu na kuendesha maisha yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania (TASAF) LADISLAUS MWAMANGA amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Tassaf imejipanga kufanya marekebisho ya mfumo wa kuwatambua wanufaika wote ambao utaweza kuwasaidia zaidi na kuwafikia kwa muda muwafaka.
Mkurugenzi huyo amewapongeza Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wao wa kufuatilia kwa karibu uendeshaji wa mfuko huo wenye malengo ya kuwasaidia wananchi wa kaya masikini .
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment