Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wananchi kulinda miundombinu inayojengwa na Serikali ili iweze kudumu kwa muda mrefu .
Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati akikamilisha ziara ya mikoa mitano ya Zanzibar ya kukagua Miradi ya maendeleo inayojengwa na Serikali kwa fedha za Mkopo wa kukabiliana na athari za ugonjwa Uviko 19 kutoka IMF Mkoa wa Kaskazin Pemba.
Amesema ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anakuwa balozi wa kulinda Miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu na kuwafaa wananchi wa vizazi vijavyo.
Amesema Serikali ina wajibu wa kujenga Miundombinu imara na ya kisasa inayoendana na wakati hali ambayo itapelekea upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wakandarasi waliopewa miradi hiyo kuhakikisha inakuwa bora kwa mujibu wa mikataba ya makubaliano na kuongeza kuwa Serikali haitahusika na hasara yoyote itakayotokana na uzembe wa wakandarasi hao.
Mhe. Hemed ameongeza kuwa ni vyema kwa wakandarasi hao kuzingatia muda wa kumaliza miradi hiyo na kuwataka kuongeza juhudi na kujiandaa kutosita kwa miradi hiyo kipindi cha Mvua kitakapofika.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuiamini Serikali yao inayoongozwa na Dkt Hussein Ali Mwinyi ambayo imebeba jukumu la kuwatumikia wananchi wake.
Wakati akihitimisha ziara yake hizo za kukagua miradi inayojengwa kwa fedha za Mkopo wa IMF Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi waliojitokeza katika ziara hizo hatua ambayo inaonesha kuunga mkono juhudi za serikali yao.
Nae waziri wa Afya Ustawi wa Jamii wazee Jinsia na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuamua kukagua miradi hiyo na kueleza kuwa hatua hiyo ni ya kupigiwa mfano.
Mhe. Mazrui pia amewataka wananchi kuiamini Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dr Mwinyi kwa mipango madhubuti iliyoweka kwa maendeleo ya wananchi wake.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe. Matari Zahor Masoud amesema Serikali ya Mkoa imekuwa ikitembelea miradi hiyo ili kuona maendeleo yake na kuahidi kuendelea kutoa mashirikiano ya kutosha katika kukamilika kwa miradi hiyo.
Abdulrahim Khamis Mussa
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
0 comments:
Post a Comment