Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuamua kuitangaza Zanzibar kupitia Vivutio vilivyopo ndani ya Mkoa huo.
Mhe. Hemed ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Mkoa wa Kaskazini Unguja na Makala ya Hazina za Kaskazini Unguja iliyofanyika katika Hotel ya Tui Blue Bahari Zanzibar iliyopo Pwani mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema Zanzibar inajivunia vivutio vingi vya kitalii ndani ya Mkoa wa Kaskazini ambavyo vinaitangaza nchi kitaifa na Kimataifa hatua ambayo inasaidia kuvutia watalii na wawekezaji kuja kwa Maslahi ya Taifa.
Mhe. Hemed amesema kuandaliwa kwa Makala ya Hazina za Kaskazini inalenga kusaidia kukuza uchumi wa Nchi pamoja na kuvisaidia vizazi vijavyo viweze kufahamu mazingira mazuri yanayoizunguka Nchini yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wakuu wa Mikoa wengine kuwa wabunifu katika Mikoa yao kwa mujibu wa Mazingira waliyonayo kwa lengo la kuisaidia Serikali katika kukuza Uchumi wa Nchi hasa eneo la Uchumi wa Buluu.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema licha ya kutangaza vivutio hivyo ni vyema kuendeleza Mila, Silka na Tamaduni ili wageni wazidi kuvutiwa na uzuri huo na kuweza kufika Zanzibar kwa utalii na uwekezaji.
Pamoja na Mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wazanzibari kuwa mabalozi wa kuitangaza Makala hiyo ili iwafikie wengi kuweza kujionea vivutio vilivyopo Zanzibar.
Aidha Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuanzisha Makala hiyo na kueleza kuwa jambo limesaidia kuitangaza Zanzibar.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Muhamed Mahmoud ameeleza kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja umebarikiwa kuwa na vivutio vingi na miundombinu ya Kitalii jambo ambalo limepelekea kuanzia kwa makala hiyo ili kusaidia kuwafikia wengi ndani na nje ya nchi kuweza kuifahamu Zanzibar.
Amesema miongoni mwa mambo yaliyomo ndani ya Mkoa huo ni eneo la Sekta ya Uchumi wa Buluu akitolea mfano Utalii, uvuvi,Ukulima wa Mwani na Gesi na mafuta jambo ambalo litasaidia wananchi wengi kujikwamua kimaisha.
Akitoa Taarifa ya kitalaamu kuhusu Makala na Tovuti hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Unguja Ndugu Makame Machano Haji amesema kuandaa kwa Makala hiyo ni kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi alilolitoa wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa ambapo aliwataka kuwa wabunifu katika maeneo yao ya kazi ili kusaidia kukuza Uchumi wa Nchi.
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment