Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewagiza viongozi na wakuu wa Taasisi za serikali kuhakikisha wanakata bima kwa vyombo vyote vinavyomilikiwa na serikali.
Mhe. Hemed alieleza hayo katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Bima Zanzibar hafla ambayo imefanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar ilioambatana na kukabidhiwa kwa hundi ya fedha ya Shillingi Millioni Mia Moja Kumi na Tisa (119,000,000/=) Pamoja na vifaa mbali mbali kwa ajili ya skuli za Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa, serikali haitosita kumchukulia hatua mtendaji yoyote pindi chombo cha serikali kitapata ajali kutokana na uzembe wa maksudi wa kutovikatia Bima vyombo vya serikali.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais aliziagiza taasisi za Serikali na binafsi kutumia huduma za bima ipasavyo kupitia kampuni za bima zilizosajiliwa kwa kundosha udanganyifu.
Alisema ni vyema kwa taasisi hizo kujisajili katika kampuni hizo ili kukabiliana na majanga mbali mbali ambayo yanaweza kusababisha athari kwa mtu mmoja mmoja na mali zao kwa ujumla.
Mhe. Hemed alisema bima ina umuhimu mkubwa katika ustawi wa jamii na taifa lolote Duniani katika kukuza uchumi wa Nchi husika kupitia dhana nzima ya ukusanyaji wa kodi kutoka katika kampuni hizo.
Mhe. Hemed aliziagiza Taasisi za Bima kuzingatia haki na uadilifu katika kutoa fidia kwa majanga yaliyokatiwa bima pasipo na usumbufu ili kuwapa imani watumiaji na wadau wa bima.
Akigusia suala la kughushi nyaraka bandia za Bima Mhe. Hemed aliziagiza taasisi zinazosimamia sheria kama vile polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mahakama kuwa waadilifu katika kusimamia kesi za kughushi nyaraka za Serikali kwa kuwachukulia hatua kali watendaji wa vitendo hivyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitumia fursa hiyo kuzitaka taasisi nyengine kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kutimiza majukumu yao wa kutoa huduma kwa Jamii ili kuunga mkono Serikali katika kuwasaidia wananchi hususan wanaoishi katika mazingira magumu.
Mapema. Mhe. Hemed aliutaka uongozi wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali kuhakikisha fedha zilizopatikana zinatumiwa kwa uwangalifu na kufuata utaratibu wa matumizi ili kuonesha thamani halisi ya Fedha iliotumika kwa vifaa vitakavyonunuliwa.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Jamal Kassim Ali alisema uwepo wa Sekta ya bima ni moja kati ya Sekta inayosaidia kukuza uchumi wa Nchi ambapo alitumia fursa hiyo kuiopongeza mamlaka ya bima Tanzania na makampuni mengine kwa kuadhimisha hafla hiyo kwa mfumo wa kusaidia watu wenye mahitaji maalum, na kutoa wito kwa taasisi nyengine kuiga mfano huu, ili kufikia makundi mengi yenye uhitaji.
Nae Naibu Kamishna wa Bima Tanzania Bi Khadija Issa Said alieleza kuwa Tasnia ya Bima inakabiliwa na changamoto mbali mbali akitolea mfano baadhi ya Taasisi za Serikali kutotambua kampuni binafsi za bima jambo ambalo linazorotesha utendaji wa kazi zao za kila siku.
Pamoja na mambo mengine Kamishna huyo aliziomba taasisi hizo kubadili mtazamo kwa kuzitambua kampuni hizo ili kuinua ari kwa kampuni na taasisi binafsi katika kusaidia Serikali kukuza uchumi wa Nchi na kufikia maendeleo yaliokusudiwa.
Katika maadhimisho hayo Mhe. Hemed alipokea mchango wa Tasnia ya Bima nchini ikiwa ni katika kuwafariji watoto wenye mahitaji maalum katika Skuli tano za Zanzibar, mchango ambao ulipatikana katika harambee ya kuwachangia watoto hao ilyofanyika Juni 19 kupitia matembezi ya Hisani yalioshirikisha wadau na makampuni ya Bima Nchini.
Kassim Abdi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment