Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewahakishia viongozi wenye dhamana ya usimamizi wa zoezi la sensa Nchini kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirkiano katika kuhakikisha zoezi hilo lifanikiwa kwa weledi muda utakapowadia.
Mhe. Hemed alieleza hayo Ofisini kwake Vuga jijini Zanzibar ambapo Kamisaa wa sensa ya watu na makaazi Balozi Mohamed Hamza alipofika ofisini kwake akiambatana na vingozi kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu kwa ajili ya kujitambulisha kufuatia kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais aliwataka viongozi hao kuendelea kutoa elimu pamoja na kuihamasisha jamii kupitia ngazi zote kwa kuwatumia viongozi mbali mbali kupitia ngazi za Mikoa na Wilaya kwa lengo la kuwaweka wananchi tayari kuhesabiwa muda utakapofika.
Alisema zoezi hilo linalofanyika kila baada ya kipindi cha miaka kumi (10) lina umuhimu mkubwa katika kufahamu idadi ya watu wake jambo ambalo linaisaidia serikali kuweza kupanga mikakati yake ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wake.
Aidha, Mhe. Hemed aliutaka uongozi huo kuendelea kuanisha changamoto mbali mbali zinazowakabili na kuziwasilisha serikalini ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati stahiki huku akiwahakikishia Ushirikiano wa karibu akiwa Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya sensa ya watu na Makaazi.
“Napenda kuwahakikishia ushirkiano wangu, nipo tayari kushirikiana nanyi muda wowote mutakaonihitaji ili kufanikisha azma ya zoezi la kujua idadi ya watu wetu” Alisema Mhe. Hemed
Akijitambulisha mbele ya Makamu wa Pili wa Rais Kamisaa wa sensa ya watu na Makaazi Balozi Mohamed Hamza alisema anawashukuru Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa Imani yake kwake kwa kumteua kushika nafasi hiyo na kuahidi kuwa atafanya kazi zake kwa uwadilifu katika kufanikisha lengo lililokusudiwa.
Alieleza kuwa, kutokana na zoezi la sensa kuwa tegemeo la taifa atahakikisha nafasi aliokabidhiwa ya kamisaa ataitendea haki huku akifahamu jukumu lake la msingi ni kufanya uhamasishaji kwa wananchi kupitia ngazi mbali mbali.
Nae, Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi Mayasa Mahfoudh Mwinyi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa, Ofisi yake imejipanga vyema kuendesha zoezi hilo ambapo tayari imeaanda dodoso za ngazi tofauti ili kutoa fursa kwa ngazi hizo kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makaazi.
Bi Mayasa aliema zoezi la majaribio la sensa ya watu na makaazi litajumuisha jumla ya maeneo kumi katika mikoa yote ya Zanzibar.
Kassim Abdi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment