Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk.Hussen Ali Mwinyi inathamini mchango unaotolewa na viongozi wa Dini  hali inayopelekea kudumisha Amani na Utulivu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo katika mkutano uliojadili nafasi ya  viongozi wa Dini  katika kudumisha Amani na utulivu uliofanyika katika ukumbi wa shekh Idrissa Abdul Wakili kikwajuni Jijini Zanzibar.

Mhe. Hemed alisema mchango huo wa viongozi  wanaotoa kwa taifa umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kustawisha maendeleo na kuchochea ustawi wa maisha ya wananchi.

Alieleza kuwa,uwepo wa Amani na utulivu unaochangiwa na viongozi wa Dini umesaidia kuwavutia wawekezaje tofauti jambo ambalo limepelekea kwa kupatikana kwa nafasi nyingi za ajira kwa jamii na kufanikisha kufikiwa kwa lengo la Ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi 2020/2025.

Alisisitiza Hali hiyo ya Amani na Utulivu inapaswa kulindwa na kila mtu endapo kwani endapo ikipotea Serekali na Taifa kwa ujumla itashindwa kupokea watalii na wawekezaji hatimae kupunguza seheme kubwa ya Pato la Taifa.

“Nawaomba viongozi wa Dini na wananchi wote kwa ujumla tuendelee kudumisha Amani na kila mmoja wetu aendelee kuwa mlinzi wa Amani,Utulivu na mshikamano wa nchi yetu” Alisema Mhe.Hemed.

Alifafanua kwamba,viongozi wa Dini wamekuwa na moyo wa kijitolea katika kuhakikisha Amani ya Nchi inakuwepo muda wote kutokana na kazi nzuri walioifanya ya kuhakikisha Amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumzia juu ya uwepo wa Maradhi mbalimbali, Makamu wa Pili wa Rais aliwapongeza viongozi hao kwa jitihada wanazozichukukua katika kutoa Elimu kwa waumini wanao waongoza kuchukua Tahadhari dhidi ya Maradhi ya COVID -19.

“Tumeshuhudia mchango mkubwa na mikutano mbalimbali mnayoifanya katika kupambana na Maradhi ili  kuhakikisha Amani ya Nchi hii haitetereki” Alieleza Makamu wa Pili wa Rais.

Wakisilisha mada katika Mkutano huo watendaji kutoka Ofisi ya Mufti na Wizara ya Afya walieleza kwamba Jamii inapaswa kufuata miongozo na maelekezo kutoka kwa viongozi ili kufahamu usahihi wa mambo kama ilivyoelezwa kupitia kitabu kitakatifu cha Qur-ani kareem na mafundisho ya Dini nyengine kupitia miongozo ya vitabu hivyo.

Aidha, waliwataka viongozi wa Dini kutumia kutumia njia za Hekima na Busara hasa katika kukosoana kwa kutumia mafundisho ya Qur-ani na sunnah za Mtume (S.A.W.)

Akitoa salamu za shirika la Umoja wa Mataifa  linaloshughulikia watoto duniani (UNICEF) Bwana Usia Nkhoma alipongeza Serekeli ya Mapinduzi ya Zanzibar  kupitia Afisi ya Mufti kwa hatua wanazoendelea kuchukua katika kuwapatia watu  taaluma juu ya masuala mbalimbali ikiwemo elimu ya kujikinga na kipindupindu, COVID-19 pamoja na Kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.

Mwakilishi huyo wa shirika la (UNICEF)Aliwaomba viongozi wa Dini kuendelea kutoa Taaluma kwa jamii kutokana na uwezo wao walionao wa kufikisha elimu kwa waumini wanaowaongoza.

“Viongozi wa Dini sauti zenu zina nguvu kubwa kuwafikia waumini munaowasimamia,nawaombeni muendelee kutoa taaluma sambamba na nyinyi kuwa kigezo chema”Alisema Bw. Nkhoma.

Alisema UNICEF itaendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na viongozi hao kwa kutoa msaada wao wowote ule unao hitajika kwa lengo la kufanikisha adhma ya kudumisha Amani na Utulivu pamoja na kupambana na magonjwa tofauti yanayoikumba Jamii.

Kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Mhe. Mufti mkuu wa Zanzibar Shekh Saleh Omar Kabi alieleza kuwa taifa limejaaliwa Rehma na Baraka kutoka kwa Allah (S.W.) Kwa kuwa na Amani Jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa waumini na wananchi kutekeleza ibada.

Pamoja na mambo mengine Mhe.Mufti aliwakumbusha wananchi wa Zanzibar kusahau yale yote yaliopita yaliotokea katika visiwa vya Unguja na Pemba yaliosababishwa na matukio mbalimbali na badala yake aliwahimiza kuungana pamoja sambamba na kuepuka chokochoko zitakazo sababisha kusambaratisha kwa Amani na utulivu miongoni kwa waumini wake.

Kassim Abdi

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

0 comments:

 
Top