Kassim Abdi

Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Vijana nchini wametakiwa kuzingatia ushauri kutoka kwa walezi na wazazi wakati wanapotaka kufunga ndoa ili kujijengea mustakbali mwema wa maisha yao.

Khatibu Al-Ustadhi Ali Juma Mwalimu ametoa nasaha hizo wakati akiwatubia waumini walioshiriki sala ya Ijumaa katika mskiti wa Omar Bin Khatabi wa Makondeko uliopo Kinuni wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Amesema vijana wanapozingatia ushauri kutoka kwa wazazi wao kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zitakazojitokeza katika maisha ya ndoa ikiwemo kupunguza tatizo la talaka katika Jamii.

Al-Ustadi Ali Juma alitumia fursa hiyo kwa kuwaomba viongozi wa serikali kuunda mazingira mazuri kwa vijana waweze kuowa na kuolewa kwani kufanya hivyo kutasaidia kuweka Amani na utulivu kwa Ustawi wa wananchi wake.

Aidha, waumini wa mskiti huo wa Omar Bin Khatabi wamemuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kutatuliwa kwa changamoto ya ajali za mara kwa mara zinazokea mskitini hapo zinazosababishwa kukosekana kwa uwepo wa matuta.

Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimu waumini na wananchi waliotekeleza ibada ya sala ya Ijumaa katika mskiti huo amewataka wazazi kuwasimamia vijana wao katika suala zima la kutafuta elimu ili kutengeneza wataalamu watakaotoa mchango kwa taifa.

Mhe. Hemedi amesema Zanzibar inahitaji wataalamu wazawa watakaokuwa na uzalendo katika kulitumikia taifa lao kupitia Nyanja tofauti ikiwemo Nyanja ya uchumi.

“Niwaombe wazee wangu suala la elimu tulipe kipaumbele kwa vijana wetu” Alisema Makamu wa Pili

Alieleza kuwa, wazazi wanapaswa kufuatilia kwa karibu matokeo ya masomo ya watoto wao kwa lengo la kupima na kufutilia ufahamu wa vijana jambo litakalosaidia kuwaanda wataalamu mapema katika ngazi ya msingi.

“Sio jambo la kupendeza hata kidogo serikali kutegemea wataalamu kutoka nje”  Alieleza Mhe. Hemed

Mapema Asubuhi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifika katika hospital ya Rufaa ya Mnazi mmoja kuwakagua majeruhi wa ajali ya basi iliyotokea Mkoani Shinyanga,  waliowasili zanzibar jana jioni.

Makamu wa Pili  amewataka madaktari  kuendelea kuwahudumia vyema majeruhi hao ili hali zao ziweze kuimarika haraka waweze kurudi katika majukumu yao ya ujenzi wa taifa.

 


0 comments:

 
Top