Jumla ya Shilingi Milioni Tisini na Tano (95,000,000/=) zimekusanywa katika harambee ya kuchangia vifaa kwa watoto wenye Mahitaji maalum kutoka katika skuli tano za Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi aliendesha Harambee hiyo iliosimamiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba yake iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul wakili uliopo Kikwajuniu.

Akihutubia kwa Naiba ya Rais wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alisema kuwa kuwepo kwa shughuli za kijamii katika Sekta ya Bima ni chachu ya maendeleo na kuisogeza karibu zaidi Tasnia ya Bima kwa wananchi.

Mhe. Hemed aliyapongeza makampuni hayo na kueleza kuwa kitendo cha kusadia vifaa kwa watoto wenye mahitaji maalum ni cha kupigiwa mfano kwani kinalenga kutoa huduma kwa bila ya kujali utofauti wa maumbile yao.

Mhe. Hemed aliisihi jamii kuwajali zaidi watoto wenye mahitaji maalum hasa katika kuwapa kipaumbele kwenye maeneo ya huduma kama vile huduma za Afya na masuala mengine ya kijamii.

Kuhusu vifaa vya kufundishia Mhe. Hemed alieleza kuwa kuna haja ya Taasisi na Mashirika mbali mbali nchinik kuunga mkono juhudi za Serikali, ili kufikia malengo ya kuwapatia elemu bora watoto hao.

Aidha, alisema huduma za Bima ni muhimu katika maisha kwa maendeleo ya shughuli mbali mbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi pamoja kuvutia uwekezaji.

 “Kukata Bima ni sehemu muhimu katika ukuaji wa uchumi kwani kuna lenga kuwalinda wananchi dhidi ya majanga yanayoweza kuwakabili katika shughuli zao maisha ya kila siku” Alisema Mhe. Hemed

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyashukuru mashirika mbali mbali kwa kushiriki katika harambee hiyo kwa kuonesha kuguswa kwao katika kuwasaidia watoto hao na amewataka kuendeleza jitihada hizo kwa maeneo mengine mbali mbali ya kijamii yenye uhitaji.

Nae Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Bi Khadija Issa Said alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa  kuandaliwa kwa hafla hiyo  kunadhihirisha jinsi gani mamlaka za Bima zinathamini kutoa mchango wake kwa jamii, hasa watoto wenye mahitaji maalum.

Pamoja na mambo mengine, Bi Khadija alisema kuwa wamechagua eneo hilo la watoto wenye mahitaji maalum baada ya kuona uhitaji wa watoto hao katika kuwapatia vifaa mbali mbali kwa ajili ya kuendesha shughuli zao muhimu.

Katika hafla hiyo Mhe. Hemed alikabidhi vifaa mbali mbali ikiwemo mashine ya kufulia, majaba, na vifaa vya kuchezea kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alishiriki katika matembezi ya hisani ya kuchangia vifaa kwa watoto wenye mahitaji maalum yaliyoanzia Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi Squre Kisonge kupitia Ofisi za Bima Mpirani, Mnazi Mmoja na kumalizia Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni, ikiwa katika muendelezo wa wiki ya Bima Zanzibar  ambayo kilekle chake kinatarajiwa kifikia mwishoni mwa mwezi huu.

Kassim Abdi

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top