Na Jumbe Ismailly -MANYONI 

WAZIRI wa maji,Jumaa Aweso amewapongeza wahandisi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida kwa kutekeleza kwa vitendo dhana ya kumtua mama ndoo kichwani,baada ya kuokoa shilingi milioni 150 kwa kukamilisha mradi wa maji uliotarajiwa kugharimu shilingi milioni 350 na kuukamilisha kwa shilingi milioni 200.

Waziri Aweso ametoa pongezi hizo katika Kijiji cha Kashangu,wilayani Manyoni,Mkoani Singida baada ya kutembelea na kukagua mradi wa maji wa Kijiji cha Kashangu uliopo katika Halmashauri ya Itigi na kuridhishwa na ujenzi wa mradi huo pamoja na thamani ya fedha zilizotumika.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kashangu waliohudhuria katika hafla hiyo,Waziri huyo aliweka bayana dhamira ya wizara ya maji kwamba yeye pamoja na watendaji wa wizara hiyo hawatakuwa kikwazo cha wana Itigi,wana Manyoni na wana Singida kupata maji safi na salama na yenye kutosheleza mahitaji yao.

“Ambacho nachotaka kuwaambia wana Manyoni,ambacho nachotaka kuwaambia wana Itigi,mimi Jumaa Aweso pamoja na timu yetu ya wizara ya maji hatutakuwa kikwazo kwa wana Itigi,wana Manyoni na wana Singida kupata maji safi na salama na yenye kutosheleza mahitaji yenu”alisisitiza waziri huyo huku akishangiliwa kwa makofi.

Kwa mujibu wa Awesso katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wizara ya maji iliwaagiza watalaamu wake kubadilika katika utendaji wao wa kazi kwa kuhakikisha wanapunguza gharama kubwa zinazotumika katika utekelezaji wa miradi ya maji na kuwatahadharisha kwamba atakayeshindwa kutekeleza agizo hilo atakuwa hatoshi kwenye nafasi yake.

“Nataka nifurahi na niwapongeze Ruwasa eneo hili la Manyoni na Singida yake kwa kufanya kwa vitendo,hongereni sana na mungu awabariki sana,mmetuheshimisha na hii ndiyo azma ya Rais wetu dkt John Pombe Magufuli ya kumtua mwanamama ndoo kichwani na ilani hapa ya chama cha mapinduzi imetekelezeka kwa vitendo,ccm hoyee”alisisitiza.

Hata hivyo waziri huyo alibainisha kwamba pamoja na wataalamu katika maeneo mengine wamekuwa wakichukuliwa hatua lakini kwa wataalamu wa Mkoa wa Singida wamejipanga vizuri sana,hivyo lile jinamizi lililokuwa likiwatafuna wenzao halitawafikia wataalamu wa Mkoa wa Singida.

“Lakini kwa namna ya kipekee BM kwa hapa leo naweza nikakupa lunch kwa kazi nzuri uliyoifanya na iwe mfano kwa vijana wengine,mradi huu ulitakiwa kutekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 350,lakini huyu injinia mradi huu ametekeleza kwa milioni 200”aliweka bayana Aweso.

Akimkaribisha waziri wa maji kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Kashangu,Mkuu wa wilaya ya Manyoni,Rahabu Mwagisa alikiri kwamba Halmashauri ya Itigi ina miradi mingi ya maji na kwamba kutokana na wingi huo wa miradi hivyo mpaka sasa huduma ya maji imefikia asilimia 60 kwa mjini pamoja na vijijini.

Awali katika taarifa ya utekelezaji wa mradi huo,Mhandisi wa Ruwasa wilaya ya Manyoni,Gabriel Ngongi alisema kwamba mradi huo uliokamilika kwa gharama za shilingi milioni 200 utawanufaisha jumla ya watu 2,776 na mradi huo utasaidia kuboresha kipato cha mwananchi kwa kutumia muda mfupi kupata maji safi na salama na hivyo kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji.

0 comments:

 
Top