Na Jumbe Ismailly -SINGIDA 

FAMILIA moja ya watu tisa wakazi wa Kijiji cha Minyughe,Tarafa ya Ihanja,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida wakisumbuliwa na tumbo la kuharisha na kutapika baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida,Ramadhani Kabala alithibitisha kupokea familia hiyo yenye jumla ya watu tisa Feb,23,mwaka huu majira ya saa za jioni wakitokea katika zahanati ya Kijiji cha Makilawa ambako ndiko walikoanza kupatiwa huduma za matibabu.

Aidha Mganga Mfawidhi huyo alifafanua kwamba chanzo cha ugonjwa huo wa kutapika na kuharisha ni ugali na mboga aina ya kisamvu walichokula kama mlo wa mchana kabla ya kula chakula kingine aina ya mihogo.

“Jana (juzi) majira ya jioni tumepokea wagonjwa tisa wote ni wa familia moja ambaye mwenye umri mdogo alikuwa ni binti wa miaka nane,wakiwemo wanaume watatu na wanawake sita na walikuja na shida ya tumbo kuuma,kutapika na kuharisha”alifafanua Kaimu Mganga Mfawidhi huyo.

Waliolazwa katika Hospitali hiyo ni pamoja na Katibu Jumanne (30),Samweli Lukasi (22),Janeth Robert (15),Joyce Mussa (20,Marther Robert (8)Mercia Robert (15) na Greata Ismaili (48) wote ni wakazi wa Kijiji cha Minyuge,Tarafa ya Ihanja,wilaya ya Ikungi.

Kwa mujibu wa Kabala tatizo la kuhara na kutapika lilianza siku moja kabla ya kufikishwa katika Hospitali na baada ya kufanya mahojiano nao ilionekana walikula chakula cha juzi ambacho ni kichafu na kinachoonekana kilikuwa na athari,ambacho kilikuwa ni ugali na kisamvu walichokula mchana.

Aliweka bayana kaimu mganga huyo kwamba mgonjwa wa kwanza alianza kusumbuliwa na tumbo masaa sita,yaani saa 12 za jioni baada ya kula ugali na wengine walianza kusumbulia kuumwa na tumbo saa mbili za usiku.

“Kitaalaamu tunasema food poison,kwa hiyo sana tunahisi ni food poison kwa sababu kisamvu vile vile huwa kina sumu na hivyo kutokana na maelezo yao na jinsi ambavyo tunawaangalia tunahisi zaidi inaweza kuwa ni food poison…….

Ambacho tulichokifanya wapo vizuri wamepata matibabu wamewekewa dripu na vitu vingine kubwa tutajiridhisha tu kwa sababu ni kipindi vile vile cha masika tumechukua sampuli kwa ajili ya kuangalia choo ili kujiridhisha,kwa maana ya maambukizi ya magonjwa mengine.

Hata hivyo Kabala alitumia fuirsa hiyo kutoa wito kwa wananchi Mkoani Singida kuwa waendelee kuchukua tahadhari kwa kuwa wasafi,kwani magonjwa ya tumbo yanaenda sana usafi,kwa hali hiyo watu wajitahidi kuwa wasafi katika kipindi hiki cha masika kwa kunawa maji,wanawe dawa kwa maji yanayotiririka na sabuni,lakini pia tuhifadhi vyakula vyetu katika mazingira ambayo yasipate maambukizi yeyote.

Wakiongea kwa nyakati tofauti kwenye wodi walizolazwa,baadhi ya wagonjwa hao wameushurkuru uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuwapokea na kuendelea kuwapatia huduma nzuri na zinazoridhisha zilizowawezesha kujitambua mahali walipo,licha ya awali walipofikishwa hawakuwa wakijitambua kutokana na maumivu waliyokuwanayo.

0 comments:

 
Top