Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake inayosimamia Elimu na Mafunzo ya Amali imekusudia kuimarisha Mitaala itakayokidhi mahitaji kwa lengo la kwenda sambamba na mabadiliko ya sasa ya Sayansi na Teknolojia yanayokwenda kwa kasi Duniani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo kwenye Tafrija Maalum aliyoandaliwa kwa ajili yake na Wanafunzi wenzake wa Chuo Kikuu cha Bradford cha Uingereza chenye Tawi lake Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro Tanzania na kufanyika Hapo Hoteli ya Tembo Shangani Mjini Zanzibar.

Alisema ni imani ya Serikali Kuu kuona yenyewe inaweka kipaumbele cha Elimu ili hapo baadae Taifa liweze kujitegemea lenyewe kwa kuwa na Wataalamu wa kutosha kwenye fani zote jambo litakalosaidia kuepuka Wataalamu wa Kigeni ambao wakati mwengine wanapatikana kwa masharti yasiyotekelezeka.

Mheshimiwa Hemed alisema juhudi kubwa iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba Chini ya Dr. Ali Mohamed Shein katika kuimarisha Sekta ya Elimu itaendelezwa ili ifike wakati Zanzibar izalishe Zaidi wasomi watakaokuwa na uwezo wa kuitumia Taaluma yao mahali popote Duniani.

Alisema Washirika wa Maendeleo wa ndani na Nje ya Zanzibar wamekuwa wakishuhudia uharaka wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kipindi kifupi tokea ipokee Kijiti jinsi ilivyoanza na kasi ya kuendeleza Uchumi wake kwa kuondoa uzembe na kudhibiti mianya ya Rushwa inayoviza Maendeleo ya Jamii.

Mapema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Mkoani Morogoro kinachosimamia Tawi la Chuo Kikuu cha Bradford cha Uingereza Dr. Andrew Mushi alieleza kwamba kasi ya kuwafinyanga Wanafunzi wa Elimu ya Sekondari kuelekea Vyuo Vikuu kwa kuwatayarisha kuwa Wataalamu wa baadae haina mjadala kwa Serikali.

Dr. Andrew Mushi alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba yeye, Wahadhri wenzake pamoja na wataalamu waliowazunguuka Kitaaluma katika Fani mbali mbali wako tayari kujitolea katika kusaidia ufinyanzi wa Vijana wa Kizanzibari ambao tayari wameshaonyesha muelekeo wa kutaka kulisaidia Taifa lao katika Utumishi wa Umma uliotukuka hapo baadae.

Zanzibar tayari imeshakuwa na Vyuo Vikuu Vitatu vambavyo ni  SUZA na ZU vilivyopo Tunguu pamoja na kile cha Kumbukumbu ya Abdulrahman Al- Sumait Chukwani ambavyo Viwili kati yake vimeshafikia daraja ya kutoa wahitimu wa Eimu ya Shahada ya Uzamivu yaani PHD.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top