Na Jumbe Ismailly -MKALAMA 

KUKAMILIKA kwa Hospitali ya wilaya ya Mkalama,Mkoani Singida na kuanza kutoa huduma mbali mbali za afya zimesaidia kumpunguzia,Bi Elizabeth Samweli mkazi wa Kijiji cha Nduguti,wilayani humo kutembea umbali mrefu kufuata huduma za mama na mtoto kwa mara ya kwanza tu hospitali hiyo ilipoanza kutoa huduma hizo na kujifungua watoto watatu,waliopewa majina ya viongozi wakuu wa nchi,akiwamo Dkt.John Pombe Magufuli.

Watoto hao wakiwemo wawili wa kiume na mmoja wa kike,walipatikana wakati mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge pamoja na Madiwani ikiendelea na kupewa majina ya Magufuli,Majaliwa pamoja na Samia.

Mkuu wa wilaya ya Mkalama,Mhandisi Jackson Masaka ametoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano maalumu wa kwanza wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama ulioandaliwa kwa lengo la kuwaapisha madiwani wateule,kuchagua Mwenyekiti na Makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

 “Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutupa fedha za kujenga Hospitali ya wilaya ya Mkalama,hospitali yetu ya wilaya ya Mkalama imeanza kutoa huduma kwa akina mama wanajifungua pele.”alifafanua Mkuu wa wilaya huyo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Masaka wakati wa kampeni mama huyo (Elizabeth Samwel) ni wale akina mama waliokwenda kujifungua katika Hospitali ya wilaya katika wiki ya kwanza,mama huyo alijifungua watoto watatu kwa wakati mmoja.

“Kwa hiyo mnaweza kuona hospitali yetu ilivyo na baraka sana napenda kusema pia Mheshimiwa Magufuli alivyo na baraka sana katika wilaya ya Mkalama…..tumpigie makofi mengi mheshimiwa Raisi”alisisitiza Mhandisi Masaka huku madiwani wateule pamoja na wananchi waliohudhuria mkutano huo wakimshangilia kwa vigelegele.

Aidha Mhandisi Masaka ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mkalama aliweka bayana kwamba baada ya kuwatembelea watoto wale na kumuuliza mama yao amejifungua watoto gani,ndipo alipowapa majina ya Magufuli,Majaliwa pamoja na Samia.

“Sasa nilipowatembelea watoto wale nikamuuliza mama umejifungua watoto gani,akasema watoto wa kiume wawili na wa kike mmoja mimi nikawapa majina,kwamba mmoja ni Mheshimiwa Magufuli,mmoja ni mheshimiwa Majaliwa na mwingine ni mheshimiwa Samia kwa hiyo uongozi wote wa nchi wote watatu wapo Mkalama kwa mama huyu,mama ubarikiwe sana”alisisitiza mkuu wa wilaya huyo.

Hata hivyo baada ya chereko chereko na nderemo kutoka kwa akina mama waliokuwepo ndani ya ukumbi huo wa mkutano,ndipo mkuu huyo wa wilaya alitumia fursa hiyo kumkabidhi mama watatu jumla ya shilingi 351,000/= zilizochangwa na mkuu wa mkoa wa Singida,Dkt.Rehema Nchimbi kwa kushirikiana na wadau wengine.

“Naomba sasa nije nimkabidhi mchango ambao harambee ilianzishwa na mkuu wa Mkoa wa Singida,Dkt.Rehema Nchimbi ambaye anawajali sana akina mama na pia tulichangiwa hapa na watu mbali mbali akiwemo mheshimiwa mbunge imefikia shilingi 351,000/= naamini na wadau wengine tutaendelea kumsaidia mama huyu ili aendelee kuwatunza watoto hawa na watoto wengine wote wanaozaliwa tuwatunze ili wawe na afua nzuri watimize malengo yao ya kujenga taifa letu.”aliweka bayana Mhandisi huyo.   

Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki (CCM),Francis Isack Mtinga alisisitiza kwamba kwa kuwa mama huyo ni mpiga kura wake na kwa kuwa yeye hana mtoto hata mmoja wa kike kwa hali  hiyo aliahidi kumgharamia gharama zote na msingi na za lazima mtoto huyo anayetambulika kwa jina la Samia kwa kipindi cha miaka mitano ya uwakilishi wake.

“Kwanza kwa niaba yangu binafsi na wananchi wa Mkalama tunamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuanzisha harambee hii lakini tunakushukuru na we binafsi kwa kuifikisha mimi huyu ni mwananchi wangu,mpiga kura wangu na hapa nimembeba Samia na kwa sababu mimi sina mtoto wa kike nina wa kiume watupu,huyu Samia gharama zote za msingi za lazima kwa miaka mitano ya ubunge wangu mama tuwe tunawasiliana nikusaidie gharama zake”alibainisha mbunge huyo.

Kwa upande wake mama wa watoto hao watatu,Elizabeth Samweli pamoja na kuushukuru uongozi wa Mkoa na wilaya kwa kutambua changamoto zake zinazomkabili,vile vile alitumia hafla hiyo ya kuapishwa kwa madiwani wateule kuyaomba Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na watu wengine kuendelea kumsaidia ili watoto hao waweze kukua na kupata haki yao ya kimsingi ya elimu.

0 comments:

 
Top