Wakati Taifa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania likiwa tayari limeshaingia ndani ya Mwezi wa Uchaguzi Mkuu bado baadhi ya Waumini wa Dini tofauti Nchini wanaendelea na Dua pamoja na sala za kuliombea Taifa livuke salama katika mchakato mzima wa Uchaguzi huo.
Dua Maalum iliyowakutanisha Waumini wa Dini ya Kiislamu chini ya Uratibu wa Taasisi ya Kijamii ya Step up Foundation imefanyika mara tuu baada ya mshuko wa ibada ya Sala ya Ijumaa hapo katika Kiwanja cha kufurahishia Watoto Kariakoo na kushirikisha baadhi ya Watoto Yatima wa Mikoa Mitatu ya Unguja.
Viongozi kadhaa wa Kiserikali pamoja na Taasisi za Kidini walishiriki kwenye Dua hiyo ambapo mgeni mualikwa alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambae pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza katika hafla hiyo muhimu kwa hatma ya Taifa Mgombea huyo wa Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya CCM Dr. Hussein Ali Mwinyi alisema Jamii lazima ijifunze Matatizo mbali mbali yaliyowakumba na yanayoendelea kuwatesa baadhi ya Watu wa Mataifa yaliyoipoteza Amani yao.
Dr. Hussein alisema Wananchi wanapaswa kutambua umuhimu wa Amani na Utulivu uliopo Nchini ambapo wanawajibika kusimama imara katika kuhakikisha Lulu hiyo inaendelea kudumu kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu kwa vile maisha ya kawaida bado yataendelea kuwepo.
“ Yapo baadhi ya Mataifa ulimwenguni yamepoteza Amani yao kwa sababu ya cheche ya baadhi ya Wanajamii wenzao wenye tamaa binafsi ya Mali na Uongozi na matokeo wamekabiliwa na kazi kubwa ya kuirejesha hali hiyo”. Alisema Dr. Hussein Mwinyi.
Akizungumzia masuala ya malezi ya Watoto Yatima Mgombea huyo wa Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya Chama cha Mapinduzi alitanabahisha kwamba Wazazi na Walezi Nchini bado wana dhima ya kukumbuka jukumu lao la usimamizi wa Malezi ya Watoto waliopoteza Wazazi wao.
Dr. Hussein Mwinyi alisema changamoto zinazowakumba Watoto Yatima za kukosa huduma muhimu kama Chakula, Mavazi, Sare za Skuli, unyanyaswaji wa Kijinsia, ukosefu wa Ada za Elimu ya Juu kwa wale watoto waliofaulu kuendelea na masomo yao ya Sekondari pamoja na unyang’anywaji wa Urithi mara nyingi huibuka kutokana na Watoto hao kukosa Malezi ya pamoja.
Aliipongeza Taasisi ya Kijamii ya Step Up Foundation iliyotayarisha hafla hiyo iliyowashirikisha Watoto Yatima na kukubali kuwa Mlezi wa Taasisi hiyo ili kushirikiana nayo katika kuhakikisha Watoto hao wanaondokana na changamoto zinazowakabili.
Akitoa Shukrani kwa niaba ya Washiriki wa Dua hiyo Maalum ya kuliombea Taifa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Amani Mbombea Ubunge wa CCM Jimbo la Kikwajuni Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alisema yapo matumaini makubwa ya mafanikio ya Malezi ya Watoto Yatima kutokana na dalili za ushirikiano uliojitokeza.
Mhandisi Masauni alisema uwepo wa Taasisi tofauti zilizojitokeza kuwahudumia Watoto Yatima hasa katika masuala ya sare za Maskuli, huduma za Madrasa, vyakula na hata ushirikishwaji katika michezo mbali mbali ni uthibitisho wa dalili za mafanikio hayo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment