Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Vijana Nchini kuchangamkia fursa mbali mbali  za mafunzo ya Amali zinazotolewa na Taasisi za Serikali na zile Binafsi ikiwa ndio njia pekee na mahsusi ya kuwakomboa na tatizo la Ajira liliopo Nchini.

Alisema uchangamkiaji huo wa fursa za mafunzo ni vyema ukaenda sambamba na jitihada za Wazazi na Walezi kuwashajiisha Vijana kujiunga na Mafunzo ya Amali kwa manufaa ya Maisha yao ya baadae na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza na Vijana waliohitimu Mafunzo ya ujuzi wa Ufundi katika Vyuo vya Amali kwa Unguja na Pemba kwa Mwaka 2020 hapo Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Balozi Seif Ali Iddi alisema Mhitimu wa Vyuo hivyo ana nafasi kubwa ya ajira akilinganishwa na yule aliyemaliza Chuo Kikuu ambae inampasa apambane kutafuta Kazi.

Alisema Dira ya Maendeleo Zanzibar ya Mwaka 2000 hadi 2020 iliweka shabaha ya kuongeza Ajira kwenye Sekta ya Utalii kwa asilimia 50%, Sekta ya Kilimo asilimia 25% na asilimia 30% katika Sekta nyengine mchanganyiko.

Balozi Seif alibainisha kwamba shabaha hiyo imekusudia kupunguza kiwango cha ukosefu  wa Ajira kutoka asilimia 17.1% hadi kufikia asilimia 10%  ili pia kuongeza uwezo wa watendakazi kwa nia ya kuchukuwa fursa za ajira pale zinapojitokeza.

Alieleza kwamba katika kuufanyia Kazi Muongozo wa Taifa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha Programu ya Ajira kwa Vijana inayowaongoza kubaini  mahitaji yao wenyewe kwa Sekta za uzalishaji kama vile Kilimo, Uvuvi, Ufugaji, Uhunzi, pamoja na Kazi za Sanaa na Michezo.

“ Ikeshabainika mahitaji yao kinachofuata ni kuwajengea uwezo wa kiufundi ili kukabiliana na fursa katika soko la ajira Nchini na hata Kimataifa”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Sera za Kitaifa na Kisekta zilizopo zinaonyesha jinsi Zanzibar ilivyolichukulia suala la Ajira kwa Vijana kuwa ni jambo la msingi na muhimu linalohitaji kufanyiwa Kazi kwa Umakini mkubwa.

Alisema kwa vile Serikali imeshatekeleza jukumu lake  kwa kuwapatia mafunzo Vijana hao, kinachofuata hivi sasa kwao ni kuchapa Kazi  kwa mujibu wa fani walizosomea wakielewa kwamba Kazi ni kipimo cha Utu mahali popote pale.

Balozi Seif  alifahamisha kwamba hakuna Mtu mwenye jukumu la kubadilisha ustawi wake isipokuwa yeye mwenyewe kwani maisha mazuri wakati wote yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na halali.

Alielezea matumaini yake kwamba Wahitimu hao wataondoka mafunzoni wakiwa tayari kwenda kupambana na maisha yao na kuacha fikra za kukaa vijiweni  kulalamikia ukosefu wa Ajira ambao hatimae hujiingiza katika vitendo viovu vya uvutaji Bangi na Dawa za kulevya.

Akizungumzia suala la Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Wiki ijayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza Vijana kwa ushiriki wao tulivu katika harakati za Uchaguzi ikiwa ni pamoja na Kampeni zinazofikia ukingoni.

Alisema Vijana ni sehemu kubwa ya Wananchi watakaoshiriki katika kupiga Kura kwa kuamini kwamba  wote wamejiandikisha na tayari wanavyo Vitambulisho vya kupigia Kura. Hivyo ni vyema wakaitumia Haki yao ya Kidemokrasia kwenda kuwachaguwa Viongozi watakaosimamia Maendeleo yao.

“ Ushiriki wa Vijana unaanzia katika zoezi la kupiga Kura, kuchagua Viongozi watakaokuwa na muelekeo wa kusimamia upatikanaji wa Maendeleo katika maeneo yao”. Alisema Balozi Seif.

“ Shime Vijana tukapige kura na tuchague Viongozi bora kutoka kwenye Chama Bora chenye Mfumo wa Kisayansi na uwezo katika kuongoza Nchi”. Aliendelea kusisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasisitiza Vijana wote waliofikia umri na wamejiandikisha kuhakikisha wanakwenda kupiga Kura kwa utulivu kwa kufuata maelekezo ya Tume zote Mbili ile ya Taifa Tanzania {NEC} na ya Zanzibar {ZEC} ili kukamilisha zoezi za upigaji kura kwa salama na Amani.

Akitoa Taarifa ya Mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Bakari Ali Silima alisema jumla ya Vijana Mia 660 kutoka Wilaya zote Kumi na Moja za Zanzibar walishiriki Mafunzo hayo yaliyolenga kuwapatia ujuzi wa kukidhi mahitaji yao ya Kimaisha.

Dr. Bakari alisema uimarishaji wa Mafunzo ya Amali chini ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar umejikita katika mfumo wa mabadiliko ya Uchumi wa Viwanda  kupitia mafunzo ya Ufundi wa vifaa vya Umeme, Ushoni, Upambaji pamoja na Useremala.

Alisema katika kuimarisha uwezo wa Vijana wanaomaliza masomo yao Nchini Mamlaka ya Mafunzo ya Amali imeongeza Programu Mpya Mwaka ujao katika Fani ya Uvuvi kwa vile Taifa tayari limeshajielekeza katika kuona Uchumi wa Buluu unaongeza kasi ya Pato la Taifa hapo baadae.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali alizipongeza Taasisi mbali mbali zile ya Umma na Binafsi kwa kuwapokea Wanafunzi hao wakati wa Mafunzo yao ya Vitendo ya Miezi Sita kitendo kilichowajengea nguvu kubwa zilizopelekea kumaliza mafunzo yao kwa ufanisi.

Hata hivyo Dr. Bakari alisema zipo baadhi ya changamoto zilizokwaza wanafunzi hao katika Mafunzo yao akizitaja kuwa pamoja na kuzuka kwa Virusi vya Corona ndani ya Mafunzo yao, utoro kwa baadhi ya Wanafunzi pamoja na ongezeko kubwa la Wanafunzi lililopelekea kukaa Majumbani.

Naye kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nd. Amour Ahmed Bakari alisema Serikali kupitia Wizara inayosimamia Vijana ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni Saba kwa ajili ya Mafunzo ya kuwajengea Uwezo wa Ajira Vijana ndani ya kipindi cha Miaka Mitatu.

Nd. Amour alisema hivi sasa tayari shilingi Bilioni Tatu zimeshatolewa katika Awamu ya Kwanza ya Programu hiyo inayotekelezwa chini ya Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Vijana alibainisha kwamba Serikali imelazimika kuwajengea uwezo Wanafunzi hao mbali ya kuwapatia Vyeti lakini imeamua kuwaongezea nguvu za Vifaa kutegemea fani walizosoma na hivi sasa vyarahani kwa wale washonaji vimeshapatikana na kupelekwa kwenye Wilaya zao kwa ugawaji rasmi.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo Waziri wa Vijana, Utamaduni,  Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume amewapongeza Wahitimu wa Mafunzo hayo ya Ujuzi wa Ufundi kwa umahiri wao wa kuiunga mkono Serikali Kuu katika Mkakati wake wa kupunguza wingi la ukosefu wa Ajira Nchini.

Balozi Karume alisema Programu iliyoanzishwa ya Ajira kwa Vijana imelenga kuongeza Uzalishaji katika Fani tofauti hasa zile za Ufundi ili Taifa pale litakapoingia vyema kwenye Uchumi wa Viwanda lisije tetereka kupata Wataalamu na Watendaji wa kusimamia Sekta hiyo ya Viwanda.

Hata hivyo Waziri huyo wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliwatahadharisha Wahitimu hao lazima wazingatie umuhimu wa  kuimarisha nidhamu wakati watakapoingia ndani ya soko la ajira ili kulinda Heshima yao na Mamlaka iliyowapatia Mafunzo hayo.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top