Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vitendo vya baadhi Watu kufanya mashambulizi dhidi ya Wananchi wasio na hatia ni jambo lililo kinyume na  Imani za Dini na hulka aliyonayo Mwanaadamu ambalo linapaswa kukemewa  wakati wote na Kila Mwanajamii.

Alisema Siasa kupitia Kampeni za Uchaguzi zinazoendelea Nchini hivi sasa sio ugomvi wa uhasama ila ni mfumo uliowekwa na Vyama vya Siasa kutangaza Sera kwa Wananchi ili waridhie na kuziunga mkono kwa kuwapa ridhaa ya kuwaongoza.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo mapema asubuhi alipofika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni kumfariji na kumpa pole Mwananchi Khatib Said aliyelazwa kwa kupatiwa huduma za Afya baada ya kuchomwa kisu tumboni  na kundi la Watu waliokuwa wakirudi kwenye Mkutano wa Kampeni ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Ndugu Khatib Said alikuwa Miongoni mwa  Wananchi Tisa wa Kijiji cha Kwale Akiwemo pia Mwanamama Mjamzito wa Miezi Minane waliovamiwa kwa kupigwa Mawe na kuchomwa Visu na Kundi hilo la Wahuni wa Kisiasa mwishoni mwa Wiki iliyopita.

Alisema moyo wa Mwanaadamu katika mazingira ya kawaida lazima uwe na huruma wakati wote na kinyume na mfumo huo matokeo yake ni kujenga uhasama unaozaa uadui na chuki zisizokwisha katika jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi kwamba kwa vile Serikali ipo kwa ajili ya kulinda Raia na Mali zao waitumie haki yao ya Kidemokrasia ya kuwachagua Viongozi  kwenye uchaguzi ujao ili kuwasimamia katika harakati zao za Maendeleo.

Akiwapa pole Wananchi hao Wanane waliotibiwa na kurejea nyumbani hapo Mtaa wa Kwahaji Kijiji cha Kwale Shehia ya Majenzi Micheweni Babozi Seif  alisema vyombo vya Dola vinaendelea na uchunguzi kujiridhisha kwa kina katika uchunguzi wa tukio hilo ili baadae vichukuwae hatua za Kisheria dhidi ya Wale wote waliohusika.

Alisema Serikali kamwe haitamuonea Raia wake asiye na hatia lakini akaonya kwamba Mtu atakayebainika kuhusika na fujo au vurugu zozote hasa kipindi hichi cha Taifa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu kwa kutumia Vyombo vyake vya Dola haitasita kumdhibiti mara Moja muhusika wa fujo yoyote.

“ Serikali inatoa onyo la mwisho kutahadharisha kwamba Mtu atakayekwenda katika Kituo cha Kupiga Kura Tarehe 27 Oktoba ilhali anatambua kwamba hiyo ni siku Maalum kwa Watu Maalum litakalomfika asijetafuta Mtu wa kumlaumu”. Alitahadharisha Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza Wananchi hao waliofikwa na mitihani hiyo kwa ustahamilivu wao waliochukuwa bila ya kurejesha mashambulizi jambo ambalo limechangia uwepo wa Amani katika Kijiji hicho.

Mapema Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Mikcheweni Dr. Mbwana Shoka Salum alisema Waathirika hao Tisa walipokewa Hospitalini hapo na kupatiwa huduma za Matibabu na wengine Manane kuruhusiwa kurejea Nyumbani kuendelea na harakati zao za Kimaisha.

Dr. Shoka alisema Mgonjwa Khatib Said walilazimika kuendelea kumpa uangalizi  wa Afya baada ya kuchomwa Kitu chenye Ncha Kali Tumboni na baadhi ya chango zake kutoka Nje ambapo walilazimika kumfanyia upasuaji na hivi sasa hali yake imeleta matumaini makubwa.

Aliipongeza Serikali Kuu kupitia Wizara ya Afya kwa hatua iliyochukuwa ya kuiongezea Vifaa Hospitali hiyo ambayo kwa sasa wanaendesha shughuli za Upasuaji zilizofikia idadi ya Wagonjwa 500 ambao wangelazimika kupelekwa Hospitali ya Chake chake au Mkoani kwa matibabu zaidi.

Hata Hivyo Daktari dhamana  huyo wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni aliikumbusha Serikali na Wizara ya Afya kuzingatia upatikanaji wa vile vifaa na Zana zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi kwa vile tayari limeshajengwa Jengo Maalum la shughuli za Upasuaji.

Dr. Shoka alimuhakikishia Balozi Seif kwamba kutokana na afya ya Mgonjwa Khatib Saidi kutengamaa wakati wowote kuanzia sasa wanaweza kumruhusu kurejea Nyumbani na kumshauri apate mapumziko kipindi hichi ili kuangalia zaidi Afya yake.

Akitoa shukrani zake na kwa niaba ya Wananchi wenzake waliopata kadhia hiyo Mgonjwa Khatib Said kupitia Balozi Seif aliiomba Serikali Kuu kupitia Vyombo vyake vya Dola kuongeza Doria Mitaani ili kuwahakikishia Usalama wao dhidi ya zile cheche zinazoashiria kutendeka hapo baadae.

Nd. Khatib alisema wapo baadhi ya Watu wanaendelea kutoa vitisho dhidi ya Wananchi Wenzao jambo ambalo kama halikudhibitiwa mapema linaweza kuleta athari hapo baadae.


Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais w Zanzibar

0 comments:

 
Top