Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi wa Jamii katika baadhi ya maeneo Nchini kusimamia wenyewe miundombinu ya miradi yao ya Maendeleo ni jambo la msingi katika dhana nzima ya kupunguza gharama sambamba na kuepuka urasimu wa kucheleweshwa kwa wakati iliyopangwa.

Alisema ipo mifano mingi na hai ambayo Wananchi wamekuwa wakiishuhudia ya Miradi wanayopewa kuitekeleza Wahandisi wa kigeni lakini matokeo yake huambatana na gharama kubwa zinazoweza kuepukwa na hatimae kuibua miradi mengine mipya inayoweza kuwafaidisha Wana Jamii.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wananchi wanaoizunguuka Skuli ya Sekodari ya Fujoni, walimu, Wanafunzi na Wananchi jirani wa maeneo hayo mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ukumbi wa Mitihani wa Skuli hiyo.

Ujenzi wa Ukumbi huo ni miongoni mwa Miradi ya Kijamii iliyoibuliwa na  Wananchi wenyewe wa Shehia ya Fujoni ukigharamiwa chini ya usimamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf}.

Alisema baadhi ya wahandisi wa kigeni wanaokabidhiwa tenda za Ujenzi wa Miradi ya Kijamii  wamekuwa na tabia ya ulaghai wakati wanapohitaji malipo ya kazi hizo na baadae kuwa na sababu  na visingizio visivyokwisha katika kukamilisha miradi  wanayokabidhiwa.

Balozi Seif alieleza kwamba tabia hiyo mbaya wakati mwengine huzorotesha kukamilika kwa wakati Miradi na  hatimae huleta changamoto kwa Wananchi jambo linalokwenda kinyume na mikataba iliyosainiwa kabla ya kuanza kwa Miradi husika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru na kuupongeza Uongozi wa juu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} kwa miradi uliyomzawadia  ya Ujenzi wa Majengo hayo Matatu ya Kumbi za Mitihani kama zawadi kwa kumuunga mkono kutokana na utumishi wake ndani ya Jimbo la Mahonda aliloliongoza katika kipindi cha Miaka Mitano.

Kutokana na uibuliwaji wa Miradi hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii Balozi Seif  aliwataka Wanafunzi lazima wajenge Utamaduni mzuri wa kutunza Rasilmali wanazojengewa na Jamii ili zitumike na Wanafunzi wa vizazi vya sasa na vile vijavyo.

Alisema Serikali inawajibika kuwajengea mazingira bora Watoto ili waweze kukidhi vigezo vyao vya Taaluma vinavyopaswa kuwenda kwa kasi ya sasa ya Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.

Balozi Seif Ali Iddi aliitumia fursa hiyo kwa kuwahimiza Wananchi wote Nchini kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu katika njia za Amani na Utulivu na kuwataka Wazazi na Wazee kuwaasa Watoto wao kuepuka uchawishi wa baadhi ya Wanasiasa walioshindwa kunadi Sera zao na badala yake kuanza na cheche za vurugu.

“ Asitokee kidudu Mtu akataka kuwashawishi Watu hasa Vijana wazingatie kutaka kufanya vurugu ndani ya kipindi hichi cha mpito Taifa likikaribia kufanya Uchaguzi”. Alitahadharisha Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba ni vyema Taifa likaingia kwenye zoezi la Uchaguzi kwa salama, Amani na Utulivu.

Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Ukumbi huo Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi Bwana Ali Haji Abdullah alisema Wananchi wa Shehia ya Fujoni walitafakari na kuamua kuibua Mradi wa Ujenzi wa Ukumbi wa Mitihani ili kuwaondoshea usumbufu Watoto wao.

Bwana Ali Haji alisema ujenzi wa Jengo hilo la kisasa unakwenda sambamba na Sera ya Eimu ya kuwataka Wanafunzi hasa wale wa Sekondari na Vyuo kufanya Mitihani yao katika Ukumbi Mkubwa.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali SMT na SMZ anayesimamia Mradi wa Tasaf kwa Zanzibar Nd. Khalid Bakari Amran alisema Uongozi wa Tasaf umekuwa na Utamaduni wa kuwapa fursa Wanajamii katika Shehia zao kuibua Miradi kwa mujibu wa mahitaji yao.

Nd. Khalid alisema Mradi huo wa Ujenzi wa Ukumbi wa Mitihani katika Skuli ya Sekondari Fujoni umekisiwa kugharimu Zaidi ya Shilingi Milioni Mia moja na Sita Nukta Saba hadi kukamilika kwake.

Alisema Jengo hilo lililofikia asilimia 70% ya Gharama ya Ujenzi  linatarajiwa kuhudumia Wanafunzi 300 kwa wakati Mmoja, Afisi ya Walimu, Stoo na Vyoo kwa jinsia zote kikiwemo kile cha Wanafunzi wa mahitaji Maalum.

Akitoa salamu zkwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Mkurugenzi Huduma za Jamii Miradi ya Tasaf Tanzania Nd. Anadeus Kamagange alisema Zanzibar imefanya vyema katika uendelezaji wa Miradi ya Tasaf  Nchini Tanzania.

Nd. Kamagange Tasaf katika Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili imelenga kuwekeza katika kuziwezesha Kaya Maskini  kujikimu ambapo kila Shehia itafikiwa na kupata furda ya kutekeleza Mradi utakayoteuliwa na Wanashehia wenyewe.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top