Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Wahandisi wanaopewa miradi ya Ujenzi kuhakikisha wazingatia ubora wa Miundombinu wanayoisimamia ili kuepuka hasara au maafa wakati wa matumizi wa miradi husika.

Balozi Seif  Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Wahandisi wa ujenzi wa msingi wa kupitishia Maji ya Mvua katika eneo la Mfenesini Meli Kumi  alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Mradi huo.

Alisema ipo miradi tofauti inayoanzishwa kwa nia ya kuwaondoshea shida na usumbufu Wananchi lakini matokeo yake ndani ya muda mfupi baadhi ya miradi  huleta athari na kutokidhi mahitaji halisi kutokana na kukosa kiwango kinachokusudiwa kitaalamu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wahandisi wa Ujenzi wa Mradi huo kujitahidi kutafuta mbinu za ziada katika kuona changamoto inayowakabili Wananchi wa eneo hilo ya kufurika kwa Maji ya Mvua hasa wakati wa msimu wa Masika inaondoka au kupungu.

Alisema Mfenesini ni miongoni mwa maeneo yanayokumbwa na mafuriko ya maji ya mvua za masika na hali hiyo imeongezeka mara dufu Mwaka huu kufuatia Mradi wa ujenzi mkubwa wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni.

Balozi Seif aliwapongeza Wahandisi wa Wizara ya Ujenzi na wale wa Kampuni za Kimataifa kwa jitihada kubwa wanazoendelea kuzichukuwa za kuimarisha miundombinu ya Ujenzi wa Miradi mbali mbali ya Kiaifa ambayo imesaidia kuleta Ukombozi na Ustawi wa Jamii.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe alisema Msingi huo wenye urefu wa Mita Mia 425 unatarajiwa kumwaga maji ya mvua katika eneo la bondeni.

Alisema wahandisi wamelazimika kubadilisha mfumo wa Bomba ili kutoa fursa ya mtiririko wa kasi ya maji ya Mvua sambamba na unyanyuliwaji wa Bara  bara kwa lengo la kuepuka kutuama kwa mchanga kunakosababisha Maji kuanza kusambaa   maeneo ya Mitaani.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji alibainisha kwamba Maji ni adui mkubwa wa Bara bara. Hivyo lazima uwepo utaratibu muwafaka wa kuhakikisha yanapatia njia ya kupita bila ya kuathiri upande wowote ule.

Eneo la Mfenesini Meli Kumi limekuwa na changamoto ya kufurika kwa maji ya mvua za Masika na Mwaka huu familia zaidi zililazimika kuyahama na kuyaacha makaazi yao kutokana na ongezeko kubwa la mvua hizo zilizoleta athari kubwa ya mali zao.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


0 comments:

 
Top