Viongozi wa Vyama vya Kisiasa Nchini wamenasihiwa wakati umefika kuiga mazuri yanayotekelezwa na Chama cha Mapinduzi kwenye falsafa yake ya kudumisha Amani na Utulivu katika kuwaletea Maendeleo Wananchi kupitia Ilani yake inayotekelezeka siku hadi siku.
Nasaha hizo zimetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwanadi Wagombea Ubunge, Uwakalishi na Udiwani zilizomo ndani ya Jimbo la Bububu katika Mikutano ya Kampeni za uchaguzi inayoendelea Nchini kote.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema lazima Wanasiasa wafikie pahala kuelezea Sera, Ilani na muelekeo wa namna watakavyowahudumia Wananchi katika kuwasogezea Maendeleo badala ya kujikita katika kushajiisha matusi, vurugu na kejeli dhidi ya Viongozi wenzao katika medani ya Kisiasa.
Alisema katika Dunia ya sasa inayokwenda kwa kasi ya ajabu ya sayansi na Teknolojia maovu hayapaswi kubebewa bango kwa vile huyeyusha Amani katika sekunde chache na hatimae kuzalisha chuki na uhasama usiofutika katika nyoyo za Watu.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwaomba Wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Wananchi kujiepusha na tabia ya kufuata shari zinazosambazwa na baadhi ya Watu wasiyoitakia mema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ambao wamekosa muelekeo.
Alitanabahisha kwamba Chama cha Mapinduzi hakitalipa kisasi kutokana na Viongozi wake wa ngazi ya Maskani, Tawi ,na Wilaya kushambuliwa wakati wakiwa kwenye Ibada ya sala ya Alfajiri hapo juzi na Watu waovu katika Kijiji cha Kangagani Wete Kisiwani Pemba.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Dr. Juma Abdullah Saadala {Mabodi} alisema lengo la Chama chas Mapinduzi siku zote katika kuendelea kuongoza Dola ya Tanzania limejikita katika kulinda Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Dr. Mabodi alisema Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa madhila ya mateso kwa Wananchi Wazalendo wa asili ya Visiwa hivi ndio yaliyosababisha kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioweza pia kustawisha Demokrasia ya kuwapa fursa Zaidi Wananchi kuamua masuala yanayowahusu.
Nibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar alifahamisha kwamba Chama cha Mapinduzi kitalipa tukio la juzi Kangagani kwa kura za kishindo ifikapo Tarehe 28 Oktoba 2020 ili kuzima kiburi cha baadhi ya Wanasiasa wenye mawazo ya kutaka kupewa Dola kwa njia ya uasi.
Akitoa salamu kwenye Mkutano huo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu Jimbo la Bububu Mwanasiasa Mkongwe Visiwani Zanzibar Bwana Baraka Shamte aliwaonya baadhi ya Wanasiasa Nchini katika kipindi hichi cha Kampeni kuacha tabia ya matusi ambazo zinawqeza kuharibu zoezi zima la Uchaguzi Mkuu.
Bwana Baraka Shamte alisema Wananchi wameshachoka na siasa za chuki zinazoonyesha kutaka kuleta utabaka kati ya Wananchi wa Unguja na Pemba ambao katika Historia ya Visiwa hivi haukuwepo kabisa.
Katika Kampeni hizo za Uchaguzi wa Jimbo la Bububu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Hamashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif alimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la hilo Nd. Mwantakaje Haji Juma, Mgomea Uwakilishi Nd. Mudrik Ramadhan Soraga, Diwani wa Wadi na Bububu Nd. Ramadhan Juma Mkanga na Diwani wa Wadi ya Dole Nd. Juma William Sukwa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment