Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dr. Hussein Ali Hassan Mwinyi alisema kauli moja ya wateuliwa wa chama hicho kugombea nafasi tofauti za Uongozi katika uchaguzi Mkuu ujao ndio njia pekee ya ushindi utakaoihakikisha CCM inaendelea kushika Dola Nchini.
Alisema wagombea hao wa nafasi za Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, Viti Maalum pamoja na Udiwani wanalazimika kusimamia ushindi wa Chama chao kwa kushirikisha Wanachama wote katika ndazi zao za Mashina, Matawi na Majimbo yao ili kuitekeleza vyema Katiba ya CCM inayoelekeza Ushindi wa Chama hicho ni lazima.
Dr. Hussein Ali Hassan Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wale waliopewa fursa za kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi pamoja na wale waliokosa fursa hiyo wa Majimbo na Wadi za Unguja hapo katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani Mjini Zanzibar.
Alisema Umoja ndio silaha ya kufanikisha ushindi usio na mashaka. Hivyo Chama cha Mapinduzi kimeshaelekeza Kampeni za Mwaka huu zitazingatia Zaidi kushirikishwa Wanachama wenyewe ngazi za Chini na kupunguza Mikutano mingi ya hadhara ili kile kilichoagizwa na Chama ndani ya Ilani yake kiwafikie Wanachama na Wananchi wote.
Mgombea huyo wa Urais wa Zanzibar kupitia CCM alibainisha kwamba yapo masuala mengi yaliyopangwa na kuaninishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/2025 ambayo yatahitajika kuwafikia Wananchi mahali popote walipo kwa lengo la kufahamu yale yaliyofanyika na yatakayotekelezwa katika kipindi chengine kijacho.
“ Chama kimebaini kwamba Mikutano ya ndani ni muhimu kwa vile inapata fursa pana ya kuzipeleka sera za Chama cha Mapinduzi kwa urahisi Zaidi na hatimae kuwafikia walengwa”. Asisisitiza mpeperusha bendera huyo wa Chama cha Mapinduzi.
Dr. Hussein Mwinyi aliwapongeza na kuwashukuru Wanachama wote wa Chama hicho waliotia nia ya kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi kuanzia ngazi ya Wadi, Jimbo na hata Urais jambo ambalo limeleta upendo na faraja ya kubainisha ukomavu mkubwa wa Demokrasia ndani ya Chama hicho kikongwe Barani Afrika.
Aliwaomba wale waliofanikiwa na wale ambao kura zao hazikutosha kuanza safari iliyobakia ya pamoja ili lile lengo lao ya kuona Chama cha Mapinduzi kinazidi kuimarisha mizizi ya Uongozi Nchini Tanzania linafanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Iddi Ali Ame kwa niaba ya Wenyeviti wenzake alisema Uongozi wowote wa Wanaadamu huambatana na nguvu ya Mungu ambazo yule anayekosa aelewe kwamba hiyo ni kheir yake.
Ndugu Iddi alisema wapo Viongozi mbali mbali ndani ya utumishi wa Chama na hata ule wa Serikali ambao wameshawahi kutia nia na kugombea kuteuliwa katika nafasi tofauti vipindi vilivyopita na baadhi yao kukosa fursa ya kuteuliwa na hatimae kuamua kujitenga baada ya kutokubali na maamuzi yanayotolewa.
Akizungumzia suala la Amani ya Taifa iliyopo hivi sasa Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Kaskazini alivikumbusha vyombo vya Ulinzi kuzingatia wajibu unaowakabili wa kusimamia Amani iliyopo ambayo ni miongoni mwa Tunu za Taifa.
Ndugu Iddi alisema kumbusho lake hilo limekuja kutokana na baadhi ya Wanasiasa kutumia kipindi hichi cha mpito kuelekea Uchaguzi Mkuu kuanza cheche za kutaka kuleta vurugu na vyombo vya vya Ulinzi vipo bila ya hata kuwaita kwa kuwatahadharisha kwamba vitendo vyao vinaweza kuleta athari kwa Taifa.
Akitoa nasaha kwenye Mkutano huo wa Wagombea nafasi za Udiwani, Uwakilishi Ubunge na Urais wa Zanzibar kupitia CCM Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba Vyombo vya Dola Mwaka huu havitasika kumshughulikia Mtu au Mwanasiasa ye yote atakayechochea na kusababisha uvunjifu wa Amani ya Taifa,
Balozi Seif alisema Serikali zote mbili Nchini tayari zimeshajipanga vyema kuhakikisha Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinakwenda salama ili kumpa fursa kila Mwananchi mwenye Haki ya kupiga Kura anaitumia nafasi yake ya kumchagua Kiongozi anayemfaa Kidemokrasia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM amewaasa wale watakaoshinda kwenye uchaguzi Mkuu waelewe kwamba wana dhima ya kuwatumikia Wapiga Kura wao ili kumaliza ile kiu yao iliyowasababisha kuwapigia Kura hiyo.
Balozi Seif aliwathibitishia Wagombea hao, Wanachama wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Wananchi kuwa pamoja na kwamba ameshatangaza nia ya kupumzika Utumishi wa Jimbo lakini ameahidi kwamba kazi ya Chama ataiendeleza katika muda wote wa Uhai wake.
Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa nafasi za Udiwani, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Urais kwa upande wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi mnamo Tarehe 12 Mwezi huu 2020 Katika uwanja Maarufu wa Demokrasia wa Kibandamaiti Mjini Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment