Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafungua tena kazi za uchimbaji mchanga kuanzia Jumatatu ya Tarehe 6 Machi 2017 ikilazimika kuchukuwa uamuzi mgumu wa kusimamia moja kwa moja uchimbaji huo badala ya kuwaachia Wananchi.

Alisema maamuzi hayo ya Serikali yatakwenda sambamba na utolewaji wa bei elekezi ya mchanga ili kujaribu kuzuia uharibifu wa mazingira uliokwishaathiri maeneo mengi yaliyokwishachimbwa mchanga pamoja naulanguzi wa kupita kiasi kwa wauzaji wa rasilmali hiyo.

Akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tano wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar huko Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wizara ya Kilimo itaandaa zamu za kuchimba mchanga ili kupunguza msongamano wa gari zitakazokwenda katika maeneo ya Mchanga.

Alisema zamu hizo zitawapa fursa ya siku Tatu kwa Wiki Wananchi wa kawaida kupata rasilmali hiyo ya Mchanga na Siku Mbili kwa Wiki zitazingatiwa kwa Makampuni na Taasisi za Serikali zilizopata vibali vya Ujenzi wakati Jumamosi na Jumapili zitakuwa siku za mapumziko.

Balozi Seif alisema utafiti unaendelea kufanywa na Kamati ya Wataalamu kwa kushirikiana na ile ya Mawaziri inayoshughulikia suala mchanga kujua kiwango cha mchanga kiliopo kwenye eneo la Kiwanda cha Sukari Pangatupu, Kichwele na maeneo mengi ili kubaini wingi wake na endapo utafaa kwa matumizi ya ujenzi.

Alisema Zanzibar si nchi ya kwanza kuwa na upungufu wa mchanga ambapo ipo mifano ya uhaba wa rasilmali hiyo iliyokwishajitokeza katika baadhi ya nchi duniani kama vile Malaysia, Singapore, Phillipines na Tuvalu.

Balozi Seif alieleza kwamba upo ushahidi wa wazi uliothibitisha kuzama kwa Visiwa vodogo vidogo Vitano Nchini Phillipines kufuatia wimbi kubwa la uchimbaji wa mchanga kiholela pembezoni mwa fukwe zilizokuwa zimevizunguuka Visiwa hivyo.

Alifahamisha kwamba ushibiti huo wa rasilmali ya mchanga unaweza kupelekea Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini wakavamia fukwe kuchota mchanga. Hivyo aliziomba mamlaka zote kupiga marufuku uchotaji huo ili kujiepusha na majanga na kuangamiza Visiwa hivi.

Alitahadharisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake itatoa adhabu kali kwa mtu ye yote atakayekwenda kinyume dhidi ya agizo lililotolewa na Serikali kuhusu suala zima la uchimbaji wa Mchanga.

Balozi Seif aliwaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaporudi Majimboni kuwaelimisha Wananchi wao juu ya uhaba uliopo wa mchanga unaovikabili visiwa hivi.

Aliwashauri Wajumbe hao kuandaa utaratibu maalum wa kuwapangia Wananchi wao ziara mahsusi za kwenda kuangalia hali halisi ya uharibifu wa mazingira uliokwishafanyika katika maeneo yaliyochimbwa mchanga.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi pamoja na Wiara ya Ujenzi,Mawasiliano na Ushafirishaji zitaandaa muongozi wa uingiza wa bidhaa za ujenzi ikiwemo mchanga, kokoto, kifusi na Mawe kutoka nje ya Zanzibar.

Alisema muongozo huo utakwenda sambamba na kufuatilia utaratibu uliotumika katika uuzaji wa maeneo ya Kilimo kwa ajili ya kuchimbwa mchanga ili kubaini kwa kina ujanja unaotumika kuyabadilisha matumizi ya maeneo ya Kilimo.

Akizungumzia vita dhidi ya Dawa za kulevya vilivyotangazwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alionya kwamba Zanzibar haitakua kimbilio la waendelezaji wa biashara hiyo haramu na badala yake itakuwa gereza lao.

Balozi Seif alisema vita hivyo ni vya Nchi nzima ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar. Hivyo wale wanaofikiria kwamba vita hivyo ni kwa Tanzania Bara pekee wanaelezwa bayana kuwa wamepotea njia.

Alisema Takwimu kutoka Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya zinaonyesha kwamba mwaka 2016 jumla ya kesi 37 ziliripotiwa kwenye Mahakama za Unguja na Pemba na ni Mtu Mmoja tu ndie aliyetiwa hatiani.

Alieleza kwamba kutokana na Takwimu hizo inaonyesha wazi ukubwa wa janga hilo hauendani na kasi za kuwakamata wanaoingiza dawa za kulevya nchini na kuwapa adhabu stahiki.

Balozi Seif alisema janga la Dawa za kulevya linaweza kumalizika endapo jamii mitaani itakuwa tayari kushirikiana kwa kina na Jeshi la Polisi, vyombo vyengine vya ulinzi chini ya usimamizi wa Tume ya Uratibu wa Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

Akigusia vita dhidi ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bado lipo ongezeko kubwa la vitendo hivyo vinavyoshinda kutoa matunda mazuri yaliyokusudiwa.

Alisema takwimu za vitendo hivyo viovu zilizoripotiwa kuanzia mwezi Julai hadi Septemba Mwaka 2016 zinazonyesha jumla ya matukio 218 yamewasilishwa katika vyombo vinavyohusika Unguja na Pemba.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba hali hiyo bado inatisha na kutoa ujumbe kuwa bado Jamii inahitaji kushirikiana kwa karibu kujaribu kutokomeza vitendo vya udhalilishaji vya Kijinsia hapa Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa umahiri wao wa kujadili Miswada Mitatu na baadae kupitishwa na Baraza hilo.

Aliitaja Miswada hiyo kuwa ni Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Tume ya Uchaguzi nambari 9 ya Mwaka 1992, Mswada wa Sheria ya kufuta sheria ya Nembo nambari 1 ya mwaka 1985 na Sheria ya Bendera ya Zanzibar nambari 12 ya mwaka 2004 na kutunga sheria inayoweka masharti bora yanayohusiana na Bendera ya Zanzibar, Nembo ya Serikali yam APINDUZI ya Zanzibar na Wimbo wa Taifa wa Zanzibar ya Mwaka 2016 na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mswada mwengine ni Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sheria nambari 2 ya mwaka 2006.

Baraza la Wawakilishi lilipokea Ripoti 7 za Kamati za Kudumu za Baraza hilo ambazo ni Ripoti ya Kamati ya kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya mwaka 2016/2017, Ripoti ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Mwaka 2016/2017 na Ripoti ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Mwaka 2016/2017.

Nyengine ni Ripoti ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ya Mwaka 2016/ 2017, Ripoti ya Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari ya Mwaka 2016/2017,Ripoti ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Mwaka 2016/2017 pamoja na Ripoti ya Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirikia {PAC} ya Mwaka 2016/2017.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi halkadhalika pia walijadili Hoja Binafsi Mbili zilizoletwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Mh. Mohammed Said {Dimwa} inayohusu Dawa za Kulevya na ile ya Mwakilishi wa Jimbo la Kiwengwa Mh. Asha Abdalla Mussa iliyohusu uimarishaji wa mfumo mzima wa Kisheria unaoshughulikia uendeshaji wa Kesi za udhalilishaji wa Wanawake na Watoto Zanzibar.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tareje 10 Mwezi Mei mwaka 2017.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top