Joto la Sauti za Busara linazidi kupanda baada ya kutangazwa kurudi tena kwa tamasha hilo bora kabisa barani Afrika litakaloanza tarehe 9 – 12 Februari 2017.

Baada ya kupokea maombi takribani mia sita kutoka kwa wasanii wanaotaka kushiriki, waandaaji wameshachagua vikundi shiriki na kwa hakika mwezi februari wapenzi wa muziki watashuhudia wasanii mahiri watakaokutanishwa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki.

Taarifa kamili kuhusu wasanii watakaofanya maonyesho yao ndani ya tamasha la Sauti za Busara 2017 itatolewa mwezi wa kumi. Wasanii mia nne watakaokuwa kwenye vikundi arobaini watashiriki ikijumuisha majina makubwa na vijana wanachipukia kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Mozambiki, Afrika Kusini, Ghana, Gine, Kameruni na Ethiopia.

Dhima ya tamasha la mwaka 2017 ni Africa United. Kama anavyoelezea mkurugenzi wa tamasha bwana Yusuf Mahmoud, “dhumuni la Sauti za Busara ni kuwaleta watu pamoja wenye asili tofauti ili kusheherekea utajiri na muingiliano wa muziki wa Afrika. Tamasha huonyesha muziki wa laivu tu, wenye asili na ubunifu, na wenye kutoa ujumbe mahsusi kwa jamii na kuvutia unapopigwa jukwaani. Ikiwa unapigwa kwa ala tupu au uliochanganywa na umeme, tamasha hutoa vipaumbele kwa muziki wenye vionjo vya kiutamaduni”.

Aliendelea zaidi, “Muziki ni lugha ya ulimwengu, kupitia muziki dunia inaona na kutambua bara la Afrika ni lenye misimamo chanya, Afrika ni mahiri, Afrika ni tajiri kwa tamaduni zake. Tunatakiwa tuimarishe hali ya utulivu na amani kwa Afrika nzima; ni ipi njia ya kufanya zaidi ya kutumia lugha ya ulimwengu?”

Ili kuonyesha umakini katika kuiunganisha Afrika kupitia muziki, Sauti za Busara imeshatangaza nusu bei kwa wageni wote wenye uraia wa Afrika. Punguzo zaidi litapatikana kwa watanzania au wakaazi wa Afrika Mashariki.

0 comments:

 
Top