Na Jumbe Ismailly-Ikungi 
HALMASHAURI ya wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida bado inakabiliwa na changamoto juu ya vifo vya akina mama wajawazito,watoto wadogo pamoja na upungufu wa dawa kwenye vituo vya akutolea huduma. 

Akizindua uchangiaji wa damu salama,mfuko wa afya ya jamii(CHF) pamoja na daftari la ufuatiliaji akina mama wajawazito,Mkuu wa wilaya ya Ikungi,Miraji Mtaaturu alibainisha kwamba vifo vya akina mama vinaongezeka mwaka hadi mwaka . 

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya huyo kwa mwaka 2013 wilaya ya Ikungi ilikadiriwa kupoteza akina mama 79 kwa kila vizazi hai laki moja na hesabu hiyo imeongezeka na kufikia 94 kila vizazi hai laki moja kwa mwaka 2014 na katika mwaka 2015 akina mama 201 kila vizazi laki moja. 

“Hali hii haikubaliki ndugu zangu wa Minyughe na Ikungi kwa ujumla na baya zaidi matatizo yanayopelekea vifo hivyo yanatokana na sababu ambazo zinaweza kuzuilika,kwa mfano ukosefu wa damu katika vituo vya afya na kutozingatia vidokezo vya hatari tunavyoelekezwa wakati wa mahudhurio ya kliniki”alifafanua Mtaturu. 

Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya huyo licha ya matatizo ya akina mama wajawazito,vituo vya afya vile vile havina dawa za kutosha kwa sababu ya upungufu wa fedha za kuchangia gharama. 

Kwa mujibu wa ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 hadi 2020 ibara ya 49 inaelekeza serikali kuongeza huduma za aafya,kuongeza wataalaamu wa afya kwenye zahanati,vituo vya afya na Hospitali. 

“Ilani imetambua yaliyotekelezwa na serikali ya awamu ya nne katika sekta hii kama msingi wa kuendeleza juhudi za akupiga vita malaria,Ukimwi,Magonjwa yasiyopewa kipaumbele,Magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu pamoja na uboreshaji wa upatikanaji wa vifaa tiba na dawa”alibainisha Mkuu huyo wa wilaya ya Ikungi. 

Kwa upande wa Meneja wa Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya(NHIF) Mkoa wa Singida,Salumu Adamu aliweka wazi kwamba Mkutano wa Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi limepitisha sheria ndogo inayoilazimisha kila kaya kuchangia shilingi 10,000/= zitakazoiwezesha kuwapatia matibabu kwa familia ya watu sita,akiwemo baba,mama na watoto wanne wasiozidi umri wa miaka 18. 

“Sasa katika Halmashauri yetu ya wilaya ya Ikungi waheshimiwa madiwani wamepitisha kwa kauli moja kwamba kila kaya itachanga shilingi elfu kumi na itabeba family ya baba,mama na watoto wasiozidi umri wa miaka 18”alifafanua meneja huyo wa NHIF. 

Hata hivyo Meneja huyo alisema hivi karibuni NHIF imelipa zaidi ya shilingi milioni 121 kwa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kujiunga zaidi na mfuko huo.

0 comments:

 
Top