Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba kazi ya utekelezaji wa ahadi aliyotoa kwa Wananchi wa Jimbo hilo wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka uliopita itaendelea hatua baada ya hatua ili kukidhi matarajio yao.

Alisema utekelezaji huo una dhamira ya kuwaondoshea kiu waliyonayo Wananchi hao katika kutatua kero pamoja na changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maeneo yao wanayoishi.

Balozi Seif alisema hayo wakati akibabidhi vifaa vya Maabara kwa Skuli ya Sekondari ya Fujoni akitekeleza ahadi aliyowapa Wanafunzi, Walimu na Uongozi wa Kamati ya Skuli hiyo vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 25,000,000/- za Kitanzania.

Alisema wakati Viongozi na Kamati ya Skuli wakijitahidi kujenga mazingira bora ya Kielimu kazi inayowakabili wanafunzi hao kwa sasa ni kuhakikisha wanajikita zaidi katika kutafuta Elimu kwa lengo la kujijengea hatma njema ya maisha yao ya baadaye.

Mapema Balozi Seif Ali Iddi alipata wasaa wa kukagua Jengo jipya la Maabara aliloligharamia ujenzi wake katika Skuli hiyo ya Fujoni ambalo limefikia hatua nzuri katika kukamilika kwake.

Msimamizi wa Ujenzi wa Jengo hilo Ndugu Yasir De Costa alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi wake umeshakamilika kwa hatua ya awali ikiwemo uwepo wa huduma ya Maji na kilichosaliwa kwa wakati huu ni umakilishaji wa huduma za Umme kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi hao.

Ujenzi wa jengo hilo Jipya la Maabara la Skuli ya Sekondari ya Fujoni unakisiwa kugharimu zaidi ya shilingi Milioni 30,000,000/-.

Fujoni ni miongoni mwa Skuli Tatu za Sekondari zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda mbayo kutokana na juhudi za Walimu na Kamati ya Skuli tayari imebahatika kuwa na Darasa la Kumi na Nne { Form VI }.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top