Na Jumbe Ismailly-Ikungi
WAKULIMA wa mazao aina ya alzeti,karanga pamoja na ufuta katika wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida wameshauriwa kuacha kulima kilimo cha mazoea,na kisicholenga kuwaondoa kwenye umaskini uliokithiri miongoni mwao na badala yake wajenge utamaduni wa kulima mazao aina hiyo kibiashara,kwa lengo la kujiongezea kipato kwenye familia zao.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ikungi,Miraji Mtaturu kwenye mkutano maalumu kati yake na wazee maarufu wa wilaya hiyo uliolenga kufahamiana pamoja na kuzungumzia masuala mbali mbali ya shughuli za maendeleo ya wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa Mtaturu baadhi ya wakulima katika wilaya hiyo wamejenga utamaduni wa kulima kilimo cha mazoea, ambapo kwa kutumia fursa ya mkutano huo wa wazee maarufu amewasisitiza wakulima wa aina hiyo kuondokana na kilimo hicho ili kiweze kuwaondoa kwenye umaskini uliokithiri miongoni mwao.

Wakizungumzia sababu zinazochangia wananchi wa jimbo la Singida mashariki kugoma kuchangia michango mbali mbali ya kujiletea maendeleo yao,baadhi ya wawakilishi wa wazee hao walisisitiza kuwa hali hiyo inatokana na kutofahamu fedha zao wanazochangishwa zinatumika kwenye shughuli zipi.

Mmoja wa wazee hao ambaye pia ni mkazi wa Kijiji cha Kikio,Raphaeli Mtinda alikanusha kwamba watu wa jimbo la Singida mashariki hawataki kuchangia shughuli za maendeleo,bali kinachosababisha ni kuchukia vitendo vya wizi vinavyofanywa na watendaji wa vijiji na kata zao.

Aliweka bayana mzee huyo kuwa amewahi kushuhudia mmoja wa watendaji akipokea fedha za michango lakini cha kushangaza ni kutolewa risiti zisizokuwa halali kisheria na baadhi ya watendaji wanaoshirikiana na wakubwa wao wa Halmashauri.

Naye Evaristi Mughanga kutoka Kijiji cha Kikio hakuunga mkono kwamba shughuli za maendeleo zinakwamishwa na viongozi wa kisiasa,kwa kile alichodai kwamba hajawahi kuona barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami wananchi wanalazimishwa kuchangia.

“Umeongea vizuri,lakini umeongelea shule,ukaongelea zahanati,kuna vitu vingi vinavyohitajika katika nchi hii,kuna barabara ambayo ni miundombinu,kuna viwanda,kuna reli yote hayo yanahitajika ni mipango ya nchi”aliweka bayana.

Hata hivyo mzee huyo alionekana kutokubaliana na ushauri wa mkuu wa wilaya juu ya kuchangia zahanati,shule kwa nini hatukasikia siku hata moja waambiwe juu ya kuchangia ujenzi wa barabara.

Mughanga hata hivyo alikiri kuwa aliwahi kusikia kauli za Rais kuzuia michango,lakini hakusita kuhoji ni kwa nini Mkuu huyo wa wilaya anawataka wachangie michango na ushuru mdogo mdogo kwa kutumia ilani ya chama gani.

0 comments:

 
Top