Wizara ya Afya Zanzibar na Uongozi wa Jimbo la Jiangsu la Jamuhuri ya Watu wa China leo zimetiliana saini Mkataba wa kuupitia upya ule uliomaliza muda wake wa kuimarisha Mpango wa ushirikiano kati ya Zanzibar na Jimbo hilo katika kuimarisha Sekta ya Afya Zanzibar.

Mkataba huo pia umehusisha mpango wa Jimbo hilo kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuipatiaVifaa vya Hospitali, Dawa pamoja na Madaktari Mabingwa wanaoendelea kutoa huduma za Afya katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Malik Akil aliiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusaini Mkataba huo wakati Serikali ya Jimbo la Jiangsu ya China ikawakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Jimbo hilo anayesimamia Kamisheni ya Afya na uzazi wa Mpango Bibi Wang Yonghong.

Hafla hiyo fupi ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China {CCP } katika Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun na mwenyeji wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema huduma zinazotolewa na Madaktari mabingwa wa China wanaotoka katika Jimbo la Jiangsu zimeleta faraja kwa wananchi waliowengi hapa Zanzibar.

BaloziSeif alisema Timu ya Madaktari wa China wanaopangiwa kutoa huduma za afya Zanzibar kwa sasa wamekuwa familia na wananchi wa Zanzibar wanaowahudumia kwa takriban miaka 52 sasa.

Alisema Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Jimbo hilo imetoa mchango mkubwa katika kuwasaidia Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika sekta ya huduma ya Afya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia ujumbe huo wa Viongozi 17 kutoka Jimbo la Jiangsu Nchini Jamuhuri ya Watu wa China kwamba uhusiano wa kihistoria kati ya pande hizo mbili utaendelea kudumishwa kwa ustawi wa mataifa hayo mawili.

Balozi Seif kupitia ujumbe huo unaoongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China {CCP } katika Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun aliyaomba Makampuni na Taasisi za uwekezaji katika Majimbo mbali mbali nchini humo kuwekeza miradi yao hapa Zanzibar.

Alisema Zanzibar kwa sasa tayari imeshaimarisha miundombinu mbali mbali inayotoa fursa kwa wawekezaji kuanzisha miradi yao hasa katika sekta za Kilimo, Uvuvi, Utalii na Mawasiliano.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Malik Akil alisema Mkataba huo wa ushirikiano utatoa fursa kwa pande hizo mbili kufanya uhakiki kwa maeneo waliokuwa wakishirikiana.

Dr. Malik alisema zaidi ya Dola za Kimarekani Laki Mbili na Nusu zinatarajiwa kutumika katika mpango huo wa kuimarisha ushirikiano ikiwemo Timu za Madaktari wanaopangiwa kutoa huduma hapa Zanzibar.

Katika utiaji saini huo Uongozi wa Jimbo la Jiangsu pia utatoa msaada wa Tani 500 za Dawa na Vifaa vya Hospitali katika azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika Sekta ya Afya.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top