Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema ujenzi wa skuli karibu na maeneo wanaishi wananchi ndio njia sahihi itakayowalinda wanafunzi hasa watoto wa kike kupambana na changamoto zinazowakabili za udhalilishaji wa kijinsia zinaowakumba kutokana na sababu za kufuata elimu katika mafasa marefu.

Alisema yapo matokeo kadhaa dhidi ya watoto wa kike ya udhalilishaji wa kijinsia yaliyojitokea katika baadhi ya vijiji vya mbali vilivyozungukwa na maeneo hatarishi na kutoa nafasi kwa wahalifu kutekeleza dhamira yao mbaya ya kuwadhuru watoto wa kike.

Balozi Seif alieleza hayo wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto zinazozikabili skuli zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda ambapo alipata fursa ya kuzungumza na walimu, wanafunzi na wazazi wa Skuli ya msingi ya Zingwe zingwe pamoja na sekondari ya Fujoni katika mikutano tofauti.

Alisema takwinu za ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia zinaonyesha kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja unaoongoza vitendo ambavyo jamii kwa kushirikiana na viongozi wake inapaswa kukabiliana kwa nguvu zao zote.

Aliwahimiza wanafunzi hao kusoma kwa juhudi na nidhamu wakielewa kwamba asilimia 60% ya ufaulu kwenye masomo yao uko mikononi wakati msaada wa walimu wao unafikia asilimia 40% tu.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliwaasa wanafunzi wa kike wasikubali kukata masomo yao kwa sababu za ndoa na kuwaonya wazazi waachane na tamaa ya kukimbilia mahari kwa kuwaozesha watoto wao mapema kabla ya kumaliza masomo yao.

Alitahadharisha kwamba talaka za wanaume wa siku hizi ziko midomoni wala hazihitaji maandishi na ipo mifano ya wazi iliyotokea katika maeneo mbali mbali hasa wakati wa uchaguzi ambapo baadhi ya akinamama walitamkiwa kuachwa endapo watakipigia kura chama kisichopendwa na waume zao.

Katika kuunga mkono jitihada za skuli hizo Balozi Seif alichangia nauli ya shilingi Milioni Moja kama zawadi kwa walimu Watatu wanaojitolea katika Skuli ya Zingwe zingwe pamoja na vifaa vya ujenzi kuendeleza majengo na Mnara wa Tangi la Maji safi na salama.

Balozi Seif pia akaahidi kuwatafutia Vikalio 45 kwa madarasa Matatu ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni pamoja na vifaa vya michezo huku jitihada za kumaliza darasa la maabara zikiwa katika hatua za mwisho kukamilika.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Issa Juma Ali alisema Mradi wa kusaidia Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf } umeanzisha mpango maalum wa kusaidia kaya maskini nchini ukilenga zaidi katika kuwapatia unafuu wa kupata vifaa vya elimu wanafunzi hao.

Nd. Issa alisema mpango huo humuezesha mwanafunzi anayekabiliwa na mazingira magumu kuzitumia fedha hizo kwa kumpunguzia msongo wa mawazo mzazi wake anayeshindwa kumudu kumuhudumia mtoto wake kutokana na ukali wa maisha uliomzunguuka.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B” aliwanasihi wazazi wanaopata fedh za Tasaf kupitia mpango huo wa kaya maskini wazitumie vyema ili lengo lililokusudiwa katika mpango huo lifanikiwe vizuri.

Naye Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi aliwataka wananchi na hasa wana CCM wajizatiti katika kuimarisha uchumi ili waondokane na tabia ya kuomba omba yenye muelekeo wa udhalilishaji ndani yake.

Mama Asha alisema wapo baadhi ya wananchi waliowahi kupambana na vitendo vya udhalilishwaji kutokana na tabia ya omba omba na hatimae kupunguwa kwa utu na thamani yao katika jamii.

Wakati huo huo Mwakilishi huyo wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwakumbusha wana CCM kuendelea kushikamana katika kipindi hichi ili kuweka nguvu za muendelezo wa ushindi ifikapo mwaka 2020.

Akiendelea na ziara ya kutoa shukrani mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa kumpa ridhaa ya kuliongoza Jimbo hilo la Mahonda Balozi Seif alisema uchaguzi umekwisha hadi mwaka 2020 na kazi iliyopo sasa mbele ya wana CCM na wananchi wote ni kuelekeza nguvu zao katika kuimarisha miradi ya maendeleo.

Alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa Jimbo la Mahonda, kazi zitakazopewa kipaumbele katika kutekeleza ilani na sera za CCM ni kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi katika Wadi na shehia zao ndani ya Jimbo hilo.

Balozi Seif aliwaahidi wanachama na Viongozi hao wa Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo la Mahonda kuendelea kuziimarisha Ofisi za Chama cha Mapinduzi katika Matawi hayo ili zilingane na hadhi ya Chama chao.

Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi na wana CCM hao Balozi Seif alichangia fedha pamoja na Vifaa mbali mbali katika azma yake ya kutekeleza ahadi alizokuwa akizitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi ya kuomba kazi ya kuliongoza Jimbo hilo.

Balozi Seif alikabidhi vifaa vya ujenzi na fedha taslimu kwa kuendeleza ujenzi wa majengo ya Skuli ya Msingi ya Zingwe zingwe, Tawi la Chama cha Mapinduzi Zingwe zingwe, vifaa vya michezo pamoja na fedha taslimu kwa Timu ya Soka ya Fujoni Boys pamoja na vifaa vya ujenzi kwa Skuli ya Sekondari ya Fujoni.

Vifaa vyote hivyo katika miradi ya maendeleo na uimarishaji wa Ofisi za Chama cha Mapinduzi vimegharimu jumla ya shilingi Milioni Sita, Laki Tatui na Sitini Elfu { 6,360,000/- }.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top