Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipongeza Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya kisasa ya mtandao wa Mawasiliano ya ZTE kwa uamuzi wake wa kuunga mkono jitihada za Zanzibar katika mapambano dhidi ya maradhi ya kuambukiza ya Kipindupindu.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akipokea sehemu ya kwanza ya msaada wa vifaa na maji vilivyotolewa na Kampuni hiyo kwa ajili ya wajongwa wa Kipindupindu waliolazwa katika maeneo mbali mbali hapa Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi baadaye msaada huo akaukabidhi kwa Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar uliowakilishwa na Naibu Waziri wake Mh. Harous Said Suleiman akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Juma Malik Akil.

Sehemu ya pili ya msaada huo itakayotolewa baadae na Kampuni hiyo ya ZTE imekusudiwa kuwahudumia wananchi waliohifadhiwa kutokana na kuathirika na mvua kubwa za masika walioko kwenye Kambi ya skuli ya Sekondari ya Mwanakwerekwe “C”.

Balozi Seif alisema Uongozi wa Kampuni ya ZTE uliokuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika miradi ya maendeleo hasa ile ya uwekaji wa taa za bara barani zinazotumia nguvu za Jua { Solar } umeonyesha kuguswa na mtihani uliowapata baadhi ya Wananchi wa Zanzibar.

Mapema akikabidhi msaada huo wa mashuka, glavu, Maji pamoja na vifaa vyengine muhimu kwa wagonjwa hao Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya Kisasa ya mtandao wa Mawasiliano ya ZTE Nchini Tanzania Bwana Wayne Zhu alisema Zanzibar hivi sasa imekuwa mdau mkubwa wa Taasisi hiyo.

Bwana Wayne alisema Uongozi wa Taasisi hiyo una kila sababu ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusaidia miradi ya Maendeleo ikiwemo pia huduma za Kijamii zinazowagusa moja kwa moja Wananchi wake.

Akipokea msaada huo Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Harous Said Suleiman aliushukuru Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya kisasa ya mtandao wa Mawasiliano ya ZTE kwa msaada uliotoa ambao umekuja kwa wakati unaostahiki.

Mh.Haour aliuhakikishia Uongozi wa ZTE kwamba msaada waliotoa utatumika vyema ili usaidie kukidhi lengo lililokusudiwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top