Wakati Serikali ikijiandaa kushirikiana na ya sekta binafsi katika usajili wa vikundi vyote vya ujasiriamali ili viweze kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za Nchi, Wananchi na hasa Vijana wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa kupata ajira ambazo uwezo wa serikali wa kuwaajiri kwa wakati huu ni mdogo.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiyafungua maonyesho ya siku mbili ya wajasiri amali ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika katika bustani ya Mnara wa Kumbu kumbu ya Mapinduzi uliopo Muembe Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali kupitia Mfuko wa uwezeshaji iko tayari kuwadhamini wajasiri amali watakaofuzu mafunzo yao yanatolengwa kutolewa katika Wadi na shehia zote za Unguja na Pemba.

Alisema Taifa linaelewa changamoto zinazowasumbua wajasiriamali zikiwemo ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara, mitaji midogo pamoja na maeneo ya kufanyia biashara zao mambo ambayo yanachangia upatikanaji mdogo wa ufanisi wa kazi zao.

Balozi Seif alieleza kwamba changamoto hizo zitafanyiwa kazi na Serikali ili kuiwezesha sekta hiyo binafsi ya ujasiria amali kuwa kimbilio kwa vijana walio wengi hasa ikizingatiwa uhaba wa nafasi za ajira uliopo Serikalini.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua wazi kuwa wajasiriamali ni nguzo imara ya uchumi wa Taifa ikielewa kuwa sekta hiyo ndio mkombozi wa wananchi walio wengi hapa nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru Benki ya Posta Tanzania, Benki ya Wakulima Vijijini { CRDB } pamoja na mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } kwa mchango wao wa kusaidia wajasiriamali katika kutatua matatizo yao ya ukosefu wa mitaji ya kuendesha miradi yao.

Alisema mchango wa Taasisi hizo za kifedha umedhihirisha wazi jinsi zinavyothamini nguvu za Wananchi wao wenye juhudi za kujikwamua kimaisha kwa kujishughulisha na kazi halali za kujiongezea kipato.

Balozi Seif aliwapongeza waandaaji wa maonyesho hayo ya wajasiriamali yenye kuvutia ambayo yatawasaidia kuwaelimisha wale waliokuwa wazito wa kujielekeza katika jeshi hilo kubwa la wajasiriamali hapa Nchini.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania Bwana Sabasaba Moshing alisema katika kupiga vita umaskini unaooneka kuiathiri jamii kubwa Nchini Taasisi hiyo ya kifedha inaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali kwenye maeneo mbali mbali nchini kwa lengo la kukabiliana na tatizo hilo.

Bwana Sabasaba alisema Benki ya Posta Tanzania tayari imeshafungua Akauni Elfu 4,000 za vikundi vya vikoba na akauni nyengine 1,000 kwa vikundi visivyo rasmi kutekeleza azma ya Benki hiyo tokea ilipoanzishwa kwake kwa nia ya kumkomboa mwananchi.

Akitoa salamu Mwenyekiti wa Taifa wa Shirikisho la wajasiriamali Tanzania { TISF } Bwana Masoud Hassan Maftaha alisema Taasisi hiyo inatoa siku 60 kuanzia leo kuendesha mafunzo bure yatakayowajengea uwezo wa kitaaluma wajasiria amali wa Zanzibar.

Bwana Masoud alisema Tanzania sio omba omba iwapo mipango imara itadumishwa katika kuwajengea uwezo wananchi wake hasa wale walioamua kujikita katika sekta ya ujasiriamali.

Mwenyekiti huyo wa Taifa wa Shirikisho la wajasiriamali Tanzania alifafanua kwamba wajasiriamali wa Zanzibar lazima wawezeshwe ili kukidhi mahitaji yao muhimu pamoja na kwenda sambvamba na mpango huo.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa maonyesho hayo ya Wajasiri amali Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed alisema zipo taasisi nyingi zisizo za Kiserikali zilizoanzishwa Zanzibar ambazo tayari zimeshaleta faraja kubwa katika kumkomboa Mwananchi hasa Mwanamke.

Waziri Zainab aliwataka Wananchi hasa Wanawake na Vijana kuzichangamkia kwa haraka fursa zote zinazotolewa na taasisi hizo ili kukabiliana na ukali wa maisha na kupunguza umaskini.

Tanzania hivi sasa ina wanachama wa vikundi vya ujasiriamali wapatao Milioni 7,284,000 kati ya hao wanachama Laki 100,000 na vikundi vilivyosajiliwa vipatavyo Elfu 1,213 vipo Visiwani Zanzibar.

Utafiti uliofanya ndani ya vikundi vya wajasiriamali nchini umebaini kuwa wajasiri wengi wanafanya biashara zao chini ya kiwango kinachokubalika cha mtaji, ukosefu wa maeneo ya kufanyia biashara hizo pamoja na elimu duni ya kuendesha miradi wanayoianzisha.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top