Rais wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali linalosaidia Wananchi wenye kipato cha chini na wale wanaoishi katika mazingira magumu { Dina Foundation } Bwana Runne Evardsen alisema mchango uliotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuunga mkono taasisi hiyo umewawezesha kutoa huduma za kibinaadamu kwa wananchi waliowengi Visiwani Zanzibar.

Alisema mchango huo muhimu ulioleta faraja kwa watendaji wa shirika hilo umewaongezea nguvu za kuendelea kutoa huduma hasa za kiafya kwa wananchi wapatao Laki 150,000 kwenye shehia zipatazo 60 Unguja na Pemba.

Bwana Runne Evardsen alisema hayo akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Shirika hilo la Dina wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema watendaji wa Dina hivi sasa wanaendelea na mradi wa huduma za afya kwa kutumia gari Maalum ambapo kila Jumamosi huzunguuka kwa hutoa huduma za matibabu bure kwa wagonjwa katika maeneo tofauti.

Rais huyo wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali linalosaidia Wananchi wenye kipato cha chini na wanaoishi katika mazingira magumu alifahamisha kwamba malengo ya baadaye ya Taasisi hiyo ni kujenga kituo cha kudumu kama walivyofanya katika Nchi za Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo {DRC}.

Alieleza kwamba kazi hiyo imepangwa kwenda sambamba na uimarishaji wa utoaji huduma nyengine za matibabu kama Meno pamoja na kuwapatia msaada wa Baskeli Maalum Watu wenye ulemavu {Wheel Chair }.

Akitoa shukrani zake kwa huduma zinazotolewa na Shirika hilo la Dina Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushauri na ushirikiano ili kuona huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo zinawafikia Wananchi walio wengi hasa Vijijini.

Alisema Mpango unaoendelezwa na Shirika la Dina unakwenda sambamba na ile azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwapatia huduma bora za afya Wananchi wake.

Katika kuimarisha sekta hiyo Balozi Seif alifahamisha kwamba Sera ya Afya imetoa muongozo unaofahamisha vyema kuwa huduma za afya ya msingi zipatikane katika masafa yasiyozidi Kilomita Tano.

Hata hivyo Balozi Seif aliueleza Ujumbe huyo wa Shirika la Dina kuwa zipo baadhi ya changa moto zinazokwaza mpango huo lakini Serikali Kuu imejizatiti katika kuhakikisha miradi iliyoanzishwa kwa ajili ya mpango huo inafanikiwa.

Balozi Seif aliipongeza Serikali ya Norway kupitia Shirika hilo kwa jitihada inazochukuwa katika kuunga mkono harakati za Maendeleo za Wananchi wa Zanzibar.

Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali linalosaidia Wananchi wenye kipato cha chini na wanaoishi katika mazingira magumu { Dina Foundation }lenye Makao Makuu yake Nchini Norway hutoa huduma zote za afya ya msingi kutegemea mahitaji ya Wananchi wanaohusika.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top