Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema vyuo vikuu nchini, licha ya kuendelea kutoa taaluma kwa vijana wa elimu ya juu lakini bado vina wajibu na jukumu kubwa la kuhakikisha wasomi wake wanatumia vipaji vyao katika kufanya tafiti kwenye maeneo mbali mbali.

Alisema tafiti hizo zinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa wasomi wachanga wanaoanza kupata taaluma kwenye Vyuo hivyo sambamba na kuliwezesha Taifa kupiga hatua za haraka za Maendeleo.

Dr. Ali Moh’d Shein alitoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya 15 ya Wahitimu 686 wa Satashahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Elimu cha Kumbu kumbu ya Dr. Abdulrahman Al - Sumait kiliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamuwa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Alisema kuimarika kwa eneo la utafiti kutatoa fursa kwa wananchi mbali ya kupata elimu katika kiwango cha juu lakini pia watapata mbinu na maarifa ya kukabiliana na changamoto zilizowakabili maisha yao ya kila siku.

Rais wa Zanzibar alisema mchango mkubwa unaotolewa na Vyuo vikuu hapa Nchini hasa vile vyuo vikuu Binafsi umesaidia ongezeko kubwa la Walimu wa skuli mbali mbali za Sekondari hapa Visiwani.

“ Vyuo hivi vikuu tayari vimeshazalisha idadi kubwa ya wahitimu ambao kwa sasa wanatoa taaluma katika masomo tofauti kwenye skuli mbali mbali hapa nchini ”. Alisema Dr. Shein.

Aliushauri Uongozi wa Vyuo vikuu vya Zanzibar kuendelea kushirikiana pamoja katika kubadilishana uzoefu wa Kitaaluma kwa lengo la kuwajengea mazingira bora Walimu pamoja na Wanafunzi wa vyuo vyao.

Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba sekta ya elimu hivi sasa imepiga hatua kubwa ya mafanikio kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali Kuu kufungua milango kwa wawekezaji binafsi kuwekeza miradi yao ya elimu.

Akizungumzia suala la ushiriki wa wanafunzi wa kigeni katika vyuo vikuu vya hapa Nchini Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein aliuomba Uongozi wa vyuo hivyo kuandaa mazingira bora yatakayotoa ushawishi kwa wanafunzi wageni kupenda kupata taaluma katika vyuo Vikuu hivyo.

Alisema licha ya vyuo hivyo kukabiliwa na changamoto ya fedha katika uendeshaji wao na kulazimika kuhudumia wanafunzi wazalendo lakini bado upo umuhimu wa kuona wanafunzi wa kigeni hasa katika mwambao wa Afrika Mashariki wanajiunga na vyuo hivyo.

Dr. Shein alifahamisha kwamba kuongezeka kwa soko la Wanafunzi wa Kimataifa katika vyuo Vikuu vya Tanzania ndio njia muwafaka na muhimu katika kuvifanya vyuo Vikuu hivyo kuwa na uwezo mzuri kiufundishaji katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwashauri wahitimu hao wa chuo Kikuu cha Elimu cha Kumbu kumbu ya Dr. Abdulrahman Al Sumait chukwani kuhakikisha kwamba taaluma waliyoipata inawafaidisha katika kujiendeleza kiajira badala ya kusubiri ajiza za Serikali kuu.

Alisema katika kukabiliana na uhaba wa ajira kazi ya wahitimu hao kwa sasa ni kutafuta mbinu na maarifa yatakayowasaidia kujiendesha kiuchumi na Serikali itakuwa tayari kuwaunga mkono katika uwezeshaji wa hatma yao ya baadaye.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaandaa na kuunda mfuko Maalum wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unaolenga kutoa mikopo kwa vijana au Wananchi walioamua kuanzisha vikundi na miradi ya kujikimu kimaisha kupitia vyama vya ushirika, saccos na Vikoba.

Mapema Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Kumbu kumbu ya Dr. Abdulrahman Al Sumait Chukwani Profesa Hamed Rashid Hikmany alisema kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa chuo hicho mwaka huu kimeongezeka mara dufu kutokana na mikakati mizuri iliyowekwa na Uongozi wa Chuo hicho.

Profesa Hikmany alisema malengo ya uongozi wa chuo hicho kwa sasa ni kuimarisha zaidi utoaji wa wanafunzi wenye kiwango bora zaidi utakaokidhi mahitaji ya taaluma kimataifa.

Alisema ubora huo wa wanafunzi utaimarishwa na kwenda sambamba na walimu pamoja na watumishi wa chuo hicho kuendelea kupatiwa mafunzo yatakayokidhi mahitaji halisi ya wanafunzi wao.

Akitoa salamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Elimu cha Kumbu kumbu ya Dr. Abdulrahman Al - Sumait, Dr. Abdulrahman Al - Muhailan alisema Uongozi wa Chuo hicho utaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Sekta ya Elimu.

Dr. Al - Muhailan alisema hatua hii inalenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Kuweit kupitia sekta za mendeleo na ustawi wa jamii ambazo tayari zimeshaleta mafanikio makubwa kwa pande hizo mbili rafiki.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo Kikuu cha Elimu cha Kumbu kumbu ya Dr. Abdulrahman Al - Sumait alieleza kwamba Wananchi wa Kuweit na Zanzibar wana wajibu wa kubadilika kitaaluma kulingana na mfumo wa dunia uliopo hivi sasa wa Sayansi na Teknolojia.

Jumla ya wanafunzi 686 wa fani za Sayansi, Sanaa, Lugha ya Kiswahili, Kiarabu mfunzo ya Dini ya Kislamu wamehitimu mafunzo yao na kukabidhiwa stashahada ya kwanza.

Katika hafla hiyo Mgeni rasmi alikabidhi zawadi maalum kwa wahitimu bora zaidi sita wa daraja la kwanza katika kila fani hizo ambao ni pamoja na Moffat James Muusa masomo ya Kingereza na Geography, Haji Mohammed Haji masomo ya Kiarabu na Dini na Chabaga Masoud Chabaga masomo ya Fizikia na Kemia.

Wengine ni Muhitimu Nuru Ally Nassor Muhanna masomo ya Kiarabu na Dini, Awami Awesu Fumu masomo ya Biology na Geography pamoja na Khadija Abdulrahman Rajab masomo ya Kiarabu na Kiislamu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top