Na Jumbe Ismailly-Itigi
ZAIDI ya wakazi 23,000 wa kata ya Mitundu,tarafa ya Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida wametishia kuihama Halmashauri hiyo na kuhamia Halmashauri ya wilaya ya Sikonge,Mkoani Tabora endapo makao makuu ya Halmashauri hiyo hayatakuwa kwenye kata ya Mitundu.

Wakazi hao wametoa tamko hilo kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na diwani wa kata hiyo,Andrea Madole Mkwava kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua pamoja na kujadiliana sababu za kata ya Itigi kuwa makao makuu ya Halmashauri badala ya kata ya Mitundu kutokuwa makao makuu ya Halmashauri hiyo.

Aidha katika mkutano huo uliokuwa chini ya mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata hiyo,wakazi hao walifafanua kwamba hawaoni maana yeyote ya kudanganywa katikati ya Halmashauri hiyo ni Mji mdogo wa Itigi,wakati wananchi wa kata za Rungwa,Mwamagembe na Kintanula watakuwa bado wanafuata huduma za kijamii umbali mrefu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkutanoni hapo,wakazi hao,Sidney David Polepole alibainisha kuwa serikali iliona umuhimu wa kuigawa wilaya ya Manyoni kutokana na ukubwa wake iliokuwepo,lakini cha kushangaza watendaji wa wilaya ya Manyoni wametoa upendeleo kwa mji wa Itigi badala ya kufuata ukweli kuwa Mitundu ndiyo ingestahili kuwa makao makuu ya Halmashauri ya Itigi.

Naye Shabani Makala alisema hakuna sababu za kupiga kura za kuamua ni wapi sehemu inayostahili kuwa makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Itigi,kwani kwa ufahamu wake mdogo anaelewa kwamba agizo likitoka ngazi za juu huwa linatekelezwa tu,na kuhoji kwamba je huyo mkurugenzi anapingana na agizo la aliyekuwa waziri mkuu,Mizengo Pinda ambaye naye anatambua kuwa Mitundu ndiyo katikati ya kata zote za Halmashauri hiyo.

Kwa upande wake Habibu Ismaili aliweka wazi pia kuwa tangu mwaka 1977 wakazi wa kata hiyo wamekuwa wakiishi maisha ya ukiwa na ndicho chanzo cha manyanyaso yote wanayofanyiwa maana tangu kipindi hicho walipotembelewa na rais wa nchi mpaka leo hakuna aliyewahi kuwenda huko.

“Kutokwenda kwa Raisi kwenye maeneo hayo ya pembezoni kunakosababishwa na watendaji wa wilaya ya Manyoni kunalazimisha viongozi wakuu kutofahamu kero zao zinazowakabili na haitakuwa rahisi hata kutambua iwapo maeneo hayo kuna binadamu au wanyama peke yao ndiyo wanaoishi.”alisisitiza huku akishangiliwa na wananchi.

Graidesi Ikunya ni mkazi wa Kijiji cha Mitundu anasisitiza kuwa makao makuu ya halmashauri ya itigi haiwezekani kabisa kuwa Itigi,lakini kutokana na ukiritimba uliokuwepo siku za nyuma ndiyo ambao ulisababisha makao makuu kuwekwa Itigi.

Akizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wananchi sambamba na kuhoji uhalali wa Itigi kuwa makao makuu ya Halmashauri ya wilaya hiyo,diwani wa kata ya Mitundu,Andrea Madole Mkwava alisema kwa mujibu wa maelezo ya diwani aliyemaliza muda wake ni kwamba kutokana na ukubwa wa wilaya hiyo walipendekeza waombe wilaya na makao makuu yawe Mitundu,lakini baada ya kupatikana maamuzi yao yamebadilishwa.

0 comments:

 
Top