Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika sasa katika kuona Wananchi wanalazimika ipasavyo kutoa mashirikiano ili kusaidia kufanikisha ile azma ya Serikali Kuu ya kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya Nchini.

Alisema kukosekana ushirikiano katika kutoa ushahidi Mahakamani dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na dawa za kulevya ambako kunawahusu zaidi Wananchi walio karibu na wahusika hao inapelekea kufutwa kwa kesi na hivyo kudumaza juhudi za Serikali katika vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha Dawa za kulevya hapo Kidimni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unaguja ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964.

Alisema suala la Dawa za kulevya hivi sasa limekuwa janga la Dunia kwa vile ni la muda mrefu na kuathiri watu wengi hasa Vijana. Hivyo udhibiti wa matumizi yake unahitaji maamuzi magumu ya Serikali pamoja na ushirikiano wa Kitaifa, Kikanda na Dunia kwa ujumla.

Balozi Seif alisema licha ya changamoto zilizopo za utekelezaji wa sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya katika kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya Nchini, lakini Serikali kupitia vyombo vyake vya dola imefanikiwa kuwakamata wahusika wa biashara hiyo katika kipindi cha mwaka 2015.

Alisema Watu wapatao 48 walikamatwa na Kilo Mia 354.7 za dawa za kulevya zikiwemo bangi na heroin na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ambapo watuhumiwa wawili walifutiwa makosa yao baada ya kukosekana ushahidi, mashtaka 18 yanaendelea kusikilizwa Mahakamani na mashtaka 28 yaliyobakia yanaendelea na uchunguzi.

Balozi Seif alifahamisha kwamba suala la rushwa limekuwa likipewa nafasi kubwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya kupata mafanikio dhidi ya vita vya dawa za kulevya licha ya juhudi kubwa inayochukuliwa na Serikali katika kupambana na dhambi hiyo.

Alisisitiza kwamba mafanikio dhidi ya vita hivyo vya uzalishaji, uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya unategemea wadau wote kuanzia wananchi, taasisi binafsi pamoja na zile za umma.

“Wananchi wako karibu na maeneo yanayolimwa na kuzwa bangi, Polisi na uhamiaji wanayo nafasi kubwa ya kuwatambua wanaoingiza na kuuza dawa za kulevya, Ofisi ya Mkurugenzi mashtaka inayo wajibu wa kutayarisha hati zisizokuwa na kasoro na mahakama ina jukumu la kuharakisha kutoa hukumu stahiki kwa mujibu wa sheria “. Alisema Balozi Seif.

“ Kwa hakika kila taasisi sambamba na jamii zikiamua kuwajibika ipasavyo vita dhidi ya dawa za kulevya vitafanikiwa vyema “. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif alitoa wito kwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Tume ya Kitaifa ya udhibiti na kuratibu dawa za kulevya kuongeza juhudi katika kuwajenga uwezo wa kitaaluma watendaji ili wasimamie vizuri vituo vya kurekebishia tabia kwa vijana walioamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Alizipongeza Taasisi na watu binafsi waliojitokeza kuonyesha hisia zao juu ya kukerwa na tatizo hilo ambalo kwa akiasi kikubwa limekuwa likichangia kuathiri nguvu kazi za Taifa hili ambazo zaidi ni Vijana.

Balozi Seif alieleza kwamba hatua ya kuanzishwa Nyumba za makaazi ya Vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya maarufu Sober House ni kitendo cha kizalendo cha kupigiwa mfano ambacho hata Serikali Kuu inakithamini na kuahidi kushirikiana nao katika kuinusuru Jamii dhidi ya janga hilo thakili.

“ Kufanikiwa kwa ujenzi huu ni kuinusuru jamii yetu kutokana na matatizo mbali mbali yanayosababishwa na janga hili la dawa za kulevya. Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wananchi pamoja Taasisi nyengine ziendelee kutoa ushirikiano utakaosaidia kukamilika kwa kituo hicho “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi walioanzisha nyumba hizo pamoja na Vijana wanaoishi kwenye nyumba hizo kujitahidi kutoshawishika kurudi nyuma kwa kujiingiza tena katika janga la matumizi ya dawa za kulevya.

Mapema akitoa Taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr.Omar Dadi Shajak alisema ujenzi wa kituo hicho unagharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa zaidi ya Shilingi Bilioni Nne na Milioni Mia Mbili { 4,200,000,000/- } hadi kukamilika kwake.

Dr. Shajak alisema Kituo hicho cha aina yake ndani ya ukanda wa Mwambao wa Afrika Mashariki kitakuwa na uwezo wa kuhudumia Vijana wapato 200 wake kwa waume kwa wakati mmoja ambapo pamoja na mambo mengine kutakuwa na mafunzo ya kazi za amali, michezo na huduma nyengine za kurekebisha tabia.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshatoa jumla ya Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Tano kwa kazi za ujenzi huo kwa awamu ya kwanza inayotarajiwa kukamilika mwezi wa aprili mwaka huu na kutoa huduma mara moja.

Dr. Omar Dadi Shajak alifahamisha kwamba Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya tayari imeshaandaa zawadi kwa Mtu au Kikundi kitakachojitolea kutoa Taarifa ya kukamatwa kwa wahusika wa dawa za kulevya.

Ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha Dawa za kulevya hapo Kidimni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja chenye eneo la ukubwa wa Eka Tatu kinajengwa na Kampuni ya Kizalendo ya Al – Hilal General Trading Cooperation Limited chini ya Mkandarasi Mbwana Bakari Juma kutoka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top