Na Jumbe Ismailly-Singida 

WIZARA ya Nishati na Madini imesema itayachukua maeneo yote ya migodi ya madini yasiyoendelezwa pamoja na kufuta leseni za wamiliki wa migodo hiyo na kuigawa upya kwa makampuni na wananchi wanaoyahitaji kwa ajili ya kuyaendeleza.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dk.Medard Kalemani katika ziara yake ya siku moja Mkoani Singida ya kutembelea na kukagua miradi ya umeme vijijini (REA) ulioanza kujengwa,mwaka 2013 na ambao ulitarajiwa kukamilika,mwaka jana.

AIDHA Dk.Kalemani amesema kwa mujibu wa sheria ya madini ni kwamba Kampuni au mtu yeyote yule asiyetekeleza wajibu wake wa kuendeleza maeneo iliyochukua,hulazimika kupewa notisi ya siku 30 na baada ya kwisha leseni hufutwa na hatimaye serikali hutwaa tena eneo husika na kuligawa kwa watu wengine.

Awali akitoa taarifa fupi ya wilaya,Mkuu wa wilaya ya Manyoni,Bi Fatma Hassani Toufiq ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini ili waweze kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha
zitakazowasaidia kujiongezea mitaji pamoja na vipato vyao.

Naye Mbunge wa jimbo hilo Bwana Danieli Mtuka ametoa wito kwa serikali za vijiji unakopita mradi huo kuzilinda nguzo za umeme ambazo bado hazijachimbiwa.

Katika hatua nyingine,Naibu Waziri huyo amemwagiza meneja wa TANESCO Kanda ya kati kuhakikisha tabia iliyozoeleka ya kukatikatika kwa umeme kunakoma mara moja na pale inapobidi kukatika wasisite kutoa taarifa wizarani.

0 comments:

 
Top