Katika kipindi cha miaka kumi na mbili sasa, mwezi wa Februari umepata umaarufu kwa kujulikana kama mwezi wa Sauti za Busara, ambapo inashuhudiwa makundi ya wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wakimiminika ndani ya Mji Mkongwe kudhihirisha uwepo wa tamasha la Sauti za Busara. Takwimu za Kamisheni ya Utalii Zanzibar inaonyesha idadi ya wageni wanaokuja Zanzibar inazidi kila mwezi wa Februari, kutoka wageni 3,000 mwaka 2004 (ikiwa ni tamasha la mwanzo) mpaka wageni 40,000 kwa miaka ya hivi karibuni. Wafanyabiashara mbalimbali na hata madereva wa taxi wanakiri kwamba wiki ya Sauti za Busara ni kipindi kizuri kwao kibiashara. Mwendelezo wa hali hiyo kwa mwaka huu tunasubiri kuiona.

Mwaka jana mwezi wa nane, taasisi ya Busara Promotions ambayo inayoandaa tamasha la Sauti za Busara, ilitangaza kuahirisha tamasha la 2016 kutokana na kukosa udhamini. Mkurugenzi wa tamasha bwana Yusuf Mahmoud alisema “Mauzo ya tiketi sio tatizo, lakini mauzo hayo hufidia asilimia 30 tu ya gharama za tamasha. Ili tamasha liwe endelevu, tunahitaji kuwa na udhamini wa muda mrefu, Serikali, Wahisani wa kimataifa na wafanya biashara kubadilishana maono yetu”.

Sauti za Busara imeshaleta vikundi zaidi ya 300, vikiwemo 200 kutoka ndani ya Afrika Mashariki na vinginevyo kutoka sehemu mbalimbali za Afrika kama Madagaska, Aljeria, Mali mpaka Zimbabwe. Kwa siku nne watu takribani 20,000 uhudhuria tamasha, ikiwa ni asilimia 70 kutoka Afrika Mashariki na sehemu nyingine za Afrika na asilimia 30 kutoka Ulaya, Amerika, Mashariki ya Kati na Asia. Tamasha hutoa ajira kwa wasanii 400 na wafanyakazi 150 na kutengeneza ajira kama 2,000 kwenye sekta ya utalii Tanzania.

Maryam Hamdani, mwandishi mzuri wa nyimbo na kiongozi wa kikundi cha taarab (Tausi Women Taarab ) alisema “Nimepokea taarifa za kuahirisha tamasha kwa masikitiko makubwa. Sauti za Busara ni muhimu sana kwetu kama wasanii na vilevile kwa wapenzi wa muziki. Kwa miaka kadhaa Sauti za Busara inatutangaza na kutupa nguvu na kuonyesha kazi zetu. 
 
Tunasoma mambo mbalimbali kutoka kwa wasanii wenzetu tunaokutana nao. Vilevile tunapata faida kwa kushiriki warsha mbalimbali na kukutana na wasanii na waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali duniani, inasikitisha kwamba tutakosa fursa hizo kwa mwaka 2016. Tunaomba wadhamini walifikirie tamasha ili liweze kurudi tena mwaka 2017”.

Sauti za Busara inaiweka Zanzibar katika ramani ya kivutio cha utalii wa kiutamaduni. Hata makisio yanaonyesha tangu mwaka 2004 tamasha limeiingizia Zanzibar dola za kimarekani milioni 70. Julia Bishop, mfanyakazi wa Hotel na Mkurugenzi mstaafu wa Shirikisho la wawekezaji wa sekta ya utalii Zanzibar.
 
“ Inahuzunisha kuona tamasha ambalo linafaidisha sekta ya sanaa na utamaduni na watu wa Zanzibar kwa ujumla linaaihirishwa kutokana na ukosefu wa udhamini. zipo wapi Serikali, Mashirika na asasi zinazosema zinaunga mkono maendeleo na nani anayehitaji fursa zaidi za kujitangaza? Hili tamasha pekee linaloitangaza Zanzibar, kuonyesha vipaji vya muziki kutoka Afrika na kwingineko.”

Kwa kipindi cha mwaka mzima, Busara Promotions inahakikisha wasanii kutoka Afrika Mashariki wanapata mialiko ya kufanya maonyesho nje na kuwajengea uwezo wa kukuza ujuzi wao kupitia warsha na mafunzo ya uongozi wa sanaa. Kazi hii inadhaminiwa na Ubalozi wa Norway, Dar es Salaam ambayo haiathiriki na uamuzi wa kuahirisha tamasha la mwaka 2016.

0 comments:

 
Top