Na,Jumbe Ismailly-Singida
JESHI la polisi Mkoani Singida linawashikilia waganga wa Tiba Asili Tanzania (UWAWATA) wawili kutoka Mkoa wa Tabora na Simiyu waliokamatwa na vichwa sita vya binadamu vilivyokuwa kwenye ndoo walivyokuwa wakivisafirisha kwenda kuviuza kwa viongozi wa vyama vya siasa wa wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida.

Katibu wa Umoja wa Waganga wa Tiba Asili Tanzania(UWAWATA) Taifa,Dk.Daudi Nyaki aliyasema hayo mjini Singida kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Luluma,mjini hapa.

Aidha Dk.Nyaki alifafanua kwamba waganga hao walikamatwa kufuatia taarifa za raia wema kwamba kuna baadhi ya waganga wasiokuwa wanaotumia viungo vya binadamu kupiga ramli chonganishi na kutoa tiba zao kinyume cha sheria za nchi zinavyoelekeza.

Kwa mujibu wa katibu huyo watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na kuhojiwa walipokuwa wakivipeleka viungo hivyo vya binadamu walisema kwamba walikuwa wakienda kuviuza vichwa hivyo kwa wanasiasa waliokuwa wakishiriki kampeni za uchaguzi mkuu wa Raisi,Wabunge na Madiwani uliofanyika nchini kote Okt,25,mwaka huu.

“Hata hivyo baada ya kuwakamata mwezi wa kumi mwaka huu wakati kila chama wanachama wake walikuwa katika mchakato wa kuomba nafasi mbalimbali za uongozi,hivyo haikuwa rahisi kufahamu ni mwanasiasa yupi aliyekuwa akivihitaji viungo hivyo na kwa sababu viungo hivyo vilikuwa vikielekwa kwa waganga inakuwa siyo rahisi kumfahamu mgombea aliyekuwa na mahitaji ya viungo hivyo”alifafanua Dk,Nyaki.

Alisema umoja huo ukiwa katika operesheni maalumu ya kuwasaka na kuwakamata waganga wanaotumia viungo vya binadamu,wakitokea Mkoani Shinyanga ndipo walipofika mpakani mwa wilaya za Igunga na Iramba waliwakamata waganga wawili waliokuwa na vichwa sita vya binadamu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Hata hivyo Dk.Nyaki aliweka bayana kwamba waganga hao waliokutwa wakiwa na viungo hivyo vya binadamu wamefunguliwa mashtaka katika Mahakama ya wilaya ya Singida wakikabiliwa na tuhuma za mauaji,kesi ambayo haina dhamana.

Dk.Nyaki hata hivyo alisisitiza kwamba katika kipindi cha miezi sita sasa wamekuwa wakizunguka katika mikoa ya kanda ya kati inayohusisha mikoa ya Morogoro,Tabora,Dodoma, Singida na Shinyanga wakiunda kamati za kudhibiti vitendo vya kupiga ramli chonganishi vinavyofanywa na baadhi ya waganga wasiokuwa waaminifu.

Kwa upnde wake Mwenyekiti wa UWAWATA Mkoa wa Singida,Mohamedi Ramadhani amepiga marufuku waganga wa tiba asili waliopo katika Mkoa wa Singida,kuachana na tabia ya kubandika mabango ya matangazo ya biashara za tiba wanazotoa kwenye miti,nyumba za kulala wageni na kwenye mbao za matangazo kuanzia sasa.

“Hivyo napenda kusema na kuagiza sisi tuliofika hapa tuwe ujumbe tutakapokuta wenzetu ambao hawajahudhuria kwenye kikao hiki napenda kusema tufanyeni kazi kwa ushirikiano kwa pamoja,tufanyeni kazi kwa kupendana na tufanyenikazi kwa uaminifu”aliweka wazi mwenyekiti huyo wa UWAWATA.

Aidha mwenyekiti huyo hata hivyo hakusita kutoa onyo kwa wanachama wa chama hicho kwamba yeyote atakayebainika kuwa bado anaendelea na vitendo vya kubandika matangazo ya biashara za madawa wanayouza,chama hicho hakitasita kumchukulia hatua za kisheria,ikiwa ni pamoja na kumfungulia mara moja mashtaka Mahakamani.

“Hivyo napenda kusema na kuagiza kama mwenyekiti wa umoja huu ni mabando yanayotangaza biashara kwa waganga wa mkoa huu,hayo hatutakubaliananyo katika Mkoa huu”alisisitiza kiongozi huyo wa waganga wa asili.

Kwa mujibu wa Ramadhani kila kiongozi hana budi kuulinda utendaji wa kiongozi mwingine,na kwamba haiwezekani akaingia kiongozi wa kata kwenye kata nyingine bila kumwarifu mwenyeji wake na kwamba atakayebainika hatua kali na za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Akifunga mkutano huo,mganga mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida,Dk.Ernesti Mombeki alitumia fursa hiyo kuuagiza uongozi wa muda uliochaguliwa katika mkutano huo kuwafahamisha viongozi wengine wa vyama vya waganga wa tiba asili ili waweze kukutana dec,31,mwaka huu kwa lengo la kufahamiana pamoja na kupanga mikakati ya namna ya kufanya shughuli zao za kila siku Mkoani hapa.

Hata hivyo Dk.Mombeki alisisitiza kwamba katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa umoja wa waganga ni lazima kiongozi atakayewakilisha umoja wao awe amesajiliwa kinyume na hivyo hatakuwa tayari kumpokea na kuongeanaye,zaidi ya kumchukulia hatua za kisheria.

0 comments:

 
Top