Kampuni ya Uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi kutoka Jamuhuri ya Watu wa China iko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza miradi ya pamoja kwenye sekta hizo endapo itapatiwa fursa katika mpango wa uendelezaji wa miradi ya pamoja.

Mkuu wa Taaluma ya Miamba kutoka Kampuni hiyo ya Kimataifa ya CNOOC Bwana Cui Hanyun akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Kampunin hiyo alisema hayo wakati wa mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Cui Hanyun na Ujumbe wake ambao pia waliambatana na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yun Liang alisema Kampuni hiyo yenye kutoa huduma katika Mataifa tofauti Ulimwenguni pia inajihusisha na uwekezaji katika Benki za Ufukweni { Off Show Banking }.

Alisema Uongozi wa Kampuni hiyo umeridhika na mazingira bora yaliyopo katika Visiwa vya Zanzibar na kushawishika katika kutaka kuwekeza miradi yao ili kuunga mkono hatua za SMZ za kuwashawishi wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi kuanzisha miradi yao ya kiuchumi katika sekta tofauti Nchini.

Mtaalamu huyo wa Miamba wa CNOOC alimueleza Balozi Seif kwamba Kampuni hiyo iko tayari kuweka nguvu zaidi katika sekta ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaonyesha msisitizo kwa mujibu wa mahitaji halisi ya Taifa na Wananchi walio wengi.

Bwana Cui Hanyun alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imeshatoa baraka na kuyaruhusu Makampuni ya Nchi hiyo kuanzisha miradi ya Benki za Ufukweni kwa vile tayari imeshakuwa na wataalamu na uzoefu wa kutosha wa miaka mingi kwenye sekta hizo.

Naye Meneja wa Biashara wa Kampuni hiyo Ukanda wa Bara la Amerika Bwana Hu Gencheng alieleza kwamba Kampuni hiyo mbali ya uzalishaji pia imekuwa ikipokea Gesi kutoka Mataifa ya Indonesia, Qatar, na Autralia.

Kwa upande wa Bara la Afrika Bwana Hu Gencheng alisema CNOOC iko katika uendelezaji wa miradi ya Benki za Ufukweni katika Mataifa ya Nigeria, Equitorial Guinea, Congo Brazaville, Kenya na Uganda.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza ujumbe huo wa Kampuni ya Kimataifa ya uwekezaji wa Mafuta na Gesi ya Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajizatiti katika kutoa ushirikiano wa kina kwa Taasisi au Kampuni ye yote iliyoonyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi Zanzibar.

Balozi Seif alisema Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu jambo ambalo ushirikiano utakaotolewa kwa Kampuni hiyo ya Mafuta na Gesi ya China ni muendelezo wa uhusiano huo.

“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wa Karibu katika kuona malengo ya Kampuni ya CNOOC yanafanikiwa vyema “. Alisema Balozi Seif.

Alisema Suala la Mafuta na Gesi kwa sasa tayari limeshapatiwa maamuzi na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutolewa ndani ya Mambo ya Muungano ili kuipa fursa pana Zanzibar kushughulikia yenyewe katika dhana nzima ya kujiimarisha Kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Zanzibar itaanza matayarisho kamili ya umiliki wa Sekta hiyo pamoja na Kuunda Shirika litakaloshughulikia Sekta ya Mafuta na Gesi mara baada ya kukamilika rasmi kipindi cha mpito cha uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top