Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakamilisha taratibu zilizobakia na tayari inajiandaa kuwachukulia hatua za Kisheria watu wote waliohusika kuharibu kwa makusudi zoezi zima la Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Tarehe 25 Mwezi Oktoba mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Viongozi wa Dini mbali mbali Nchini aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kutafakari na kutafuta mbinu za kuendelea kujaribu kudumisha amani ya Nchi iliyotetereka na kuleta mtafaruku katika kipindi hicho cha Uchaguzi.

Balozi Seif alisema ina uthibitisho kamili wa vielelezo vya ushahidi wa udanganyifu kwa maeneo yote ya Zanzibar hasa katika Majimbo ya Uchaguzi ya Kisiwa cha Pemba.

Alisema Afisa wa Tume ya Uchaguzi au Mtu yoyote aliyehusika na udanganyifu huo aelewe kwamba mkondo wa sheria utamkumba kwa vile vitendo walivyofanya wameisababishia hasara kubwa Serikali pamoja wa washirika wa maendeleo walioamua kusaidia uchaguzi huo.

Balozi Seif alibainisha kwamba wakati wahusika hao wanapandishwa katika vyombo vya kisheria kujibu shutuma zinazowakabili Serikali kwa upande wake itaweka hadharani uthibitisho kamili wa vielelezo vya ushahidi wa udanganyifu huo ili Wananchi wapate fursa ya kuelewa dhambi hiyo mbaya waliyofanyiwa na watu wachache kwa tamaa binafsi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Viongozi hao wa Dini kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga vizuri kupitia vyombo vyake vya ulinzi kwa kupiga Doria maeneo yote katika kuona amani ya nchi inaendelea kudumu.

Aliwapongeza Viongozi hao wa Dini kwa jitihada zao wanazochukuwa za kutumia busara zao kwa kukutana na Viongozi wa pande mbali mbali za Kisiasa wakilenga kusaidia kutuliza mumkari na machungu ya waumini wao ambao takriban wote ni wafuasi wa vyama vya Kisiasa vilivyopo hapa Nchini.

Alivilaumu baadhi ya vyombo vya Habari hasa vile vya Nchi za Magharibi jinsi vilivyoonyesha wazi Taarifa zao nyingi wanazotowa za zoezi zima la uchaguzi Mkuu wa Zanzibar zikionyesha kuegemea upande mmoja tu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea masikitiko yake juu ya wangalizi wa Kimataifa walioamua kufuatilia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwamba hawakwenda Kisiwani Pemba muda wote wa zoezi la kupiga kura kufuatilia changamoto zilizojitokeza katika majimbo ya Pemba.

" Nimesikitishwa na waangalizi wa Kimataifa waliokuwepo Zanzibar kwa karibu mwezi mmoja kufuatilia kampeni na uchaguzi wake wameshindwa kwenda Pemba wakati wa zoezi la kupiga kura na kuonekana zaidi katika majimbo ya Kisiwa cha Unguja.

Balozi Seif aliishauri Idara ya Habari Maelezo kuendelea kufuatilia Taarifa zinazotolewa na vyombo mbali mbali vya Habari ndani na nje ya Nchini na kukemea au kutoa Taarifa dhidi ya uchochezi unaotolewa na vyombo hivyo.

Nao Viongozi hao wa Dini mbali mbali Nchini wameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua iliyochukuwa katika kusimamia amani ya Nchi.

Wananchi wa Zanzibar wamerejea katika harakati zao za kawaida za kimaisha baada ya kutokea hitilafu tofauti ndani ya zoezi zima la upigaji kura kwenye uchaguzi Mkuu wa Tarehe 25 Mwezi uliopita na kupelekea kuibuka kwa mtafaruku uliotikisa amani ya Taifa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top